Wednesday, July 25, 2012

Kubalehe

Kubalehe ni ule muda ambao mtoto wa kiume na wa kike anabadilika mwilini akielekea kuwa mwanadamu mwenye uwezo wa kuzaa.

Muda wa kubalehe ni muda ambao kunakuwa na mabadiliko kwenye mwili wa msichana au mvulana kumfanya awe mwanadamu mwenye uwezo wa kuzaa. Muda wa kubalehe yaani muda wa mabadiliko kwenye mwili wa msichana na mvulana ili kumfanya awe na uwezo wa kuzaa, huanza mapema kwa wasichana wakiwa na umri wa miaka kama kumi na kuisha wakiwa na miaka kama 14 mpaka 16. Wavulana huchelewa kidogo na huanza miaka 12 na kuisha wakifikia miaka 18. Haya ni makisio tu ya miaka maana huenda kubalehe kukaanza mapema zaidi na kuchelewa kuisha.
Kwa wasichana dalili kuwa wapo kwenye huu umri wa kubalehe, maziwa yanaanza kuwa makubwa, nywele zinaota sehemu za siri na  kwenye makwapa; wanakuwa na chunusi na baadaye wanavunja ungo yaani wanapata damu ya mwezi ya kwanza. Wavulana wanaota nywele vile kwenye sehemu za siri na kwenye makwapa, wanaota ndevu, viungo vyao vya kiume yaani korodani na uume vinakua, musuli inakuwa mikubwa na sauti inakuwa nzito.
Wakati wa kubalehe vile vile ni wakati wa kuongeza kasi ya kukua haraka haraka na kurefuka. Wanakua haraka kwa miaka kama mitatu hivyo baada ya kubalehe wanakuwa wameishafikisha karibu na urefu wao wa utu uzima.

Msichana anayebalehe
Wakati  wa kubalehe mtoto anajisikia kuwa angependa kuwa na uhuru zaidi, hujiangalia zaidi kimwili akiona jinsi anavyobadilika, huangalia mavazi anayovaa kujiweka katika hali ya kwenda na wakati na mavazi wanayovaa wenzake wa umri huo, wanaweza zaidi kuwasikiliza  vijana wakubwa na hata kukopi tabia, matendo na mavazi yao.

watoto ambao hawajabalehe
Pamoja na kukopi, kuwasikiliza na kuwadodosa wakubwa zao, wakati wa kubalehe mtoto anaendeleza uwezo na kipaji chake cha kutambua mema na mabaya. Ni wakati ambao mtoto anahitaji ukaribu na misaada ya wazazi na ya wale anaoishi karibu naye kumwezesha kujenga tabia nzuri ya kumsaidia maishani na katika utu uzima.

Tunakaribisha maswali na mawazo kuhusu kubalehe kutoka kwa vijana na wazazi. Mwandikie Mhariri bahimokahumba@yahoo.com 0712002188 au andika hapa chini.
 

YAMENIKUTA

Stori za Walioambukizwa na VVU!

1. Stori ya Yohane:
Nimekuwa na matatizo ya homa za mara kwa mara, kikohozi kikavu na ukurutu kwenye ngozi. Nilihisi labda nimeishaambukizwa VVU. Mwanzo wa mwaka huu nilijisikia kudhoofika sana.  January 25 nilienda kupima nikaambiwa nina maambukizi ya VVU. Walinipima CD4 wakakuta zimeishapungua sana na ziko 100 tu.

Nilijisikia vibaya sana. Niliomba Mungu nifie mle kliniki nilikoenda kupima lakini sikufa. Nilitoka mle nimechanganyikiwa. Nilikuwa nalia nikisema, “Nitamwambiaje mke wangu kuwa nina UKIMWI. Nitamwambiaje kuwa nimeishaambukizwa na kumwambukiza VVU?  Nilipokuwa njiani naenda nyumbani niliomba nigongwe na gari lakini magari yalikuwa yananikwepa, hayapendi kunigonga. Hakuna aliyetaka kunigonga. Nilifika nyumbani, nikampigia magoti mke wangu na  kumlilia nikimwambia, “Nisamehe mke wangu nina UKIMWI.”  Sikuthubutu kusema, “Nimekuambukiza.”  Nilimwambia tu, “Nisamehe nina UKIMWI.”

Mke wangu alisikitika na kusema, “Mume wangu, umetuua, tutakufa. Mimi nimekuwa mwaminifu kwako miaka yote hii; kumbe wewe ulikuwa unatembea nje huko.” Niliomba ardhi ipasuke inimeze lakini naona Mungu alikuwa ameishaamua kuwa ni lazima niteseke kwa muda mrefu.
Kesho yake mke wangu alienda kupima na kwa muujiza ambao mpaka sasa sijaelewa, alikutwa hajaambukizwa.
Sasa imeishapita miezi mitatu natumia dawa za kurefusha maisha. Najisikia afadhali. Kinachonipa nguvu ni sapoti ninayopata kutoka kwa mke wangu, wazazi na ndugu zangu. Wamelichukulia hiji jambo kwa kunionea huruma. Wazazi na ndugu zangu hufika mara nyingi nyumbani na kukaa na sisi na kutufariji. Nina bahati kuwa nimepata janga hili miaka hii ya karne hii. Kama ingekuwa karne iliyopita, wagonjwa kama mimi walikuwa wanatengwa na kukimbiwa na familia zao na kuwaacha wafe haraka. Sasa napewa dawa, napewa sapoti na mke wangu, wazazi na ndugu zangu. Mke wangu bado ananichukulia kama mume wake na ndugu zangu kama ndugu yao.

Nilipougua kilichonisikitisha sana ni kufikiri kuwa nitakufa kabla ya mama yaani mama atanizika. Nilianza kufikiria jinsi mama atakavyosikitika kunizika. Ninajua sasa kuwa kama nikijitahidi kujizatiti kimwili na  kimawazo nitapata afya ya kuweza kuishi na kumzika mama kuliko yeye anizike mimi. Kujitahidi kutumia dawa na kula chakula na kufanya yote ninayoambiwa na waganga na familia yangu yote  nananifanya niendelee kuishi; ili tu mama asije akanizika na baada ya hapo afe kwa uchungu wa kumzika mwanae mpenzi.

Kwa vijana ambao hawajapata maambukizi ya VVU jikingeni, jikingeni  hata kama siyo kwa faida yenu lakini kwa faida ya wazazi wenu. Inauma sana mzazi anapomzika mwanae kwa uchungu. Kawaida siyo wazazi kuzika watoto ila kwa watoto kuzika wazazi.
Tuandikie taarifa fupi jinsi unavyoteseka na UKIMWI. Tutachapisha bila jina au simu namba yako kama hutataka vitokee gazetini bahimokahumba@yahoo.com 0712002188 P.O.  Box 72321 Dar es Salaam

2. Stori ya Skolastika
Mimi naitwa Scolastica. Mwaka jana nilikuwa naumwa umwa kila mara. Nakohoa, nina homa, natoka jasho na ngozi yangu ina vipele pele. Mwezi Septemba 2011 niliamua kwenda kupima nikaambiwa nimeishaambukizwa na  VVU.  Nililia sana. Niliwafikiria wanangu. Nilijua kuwa nilikuwa nafa. Nitakufa na nitawaacha wanangu wakiteseka humu ulimwenguni. Baada ya ushauri nasaha nilijisikia afadhali, nilizoea na kuendelea kupigana na ugonjwa wangu. CD4 zilikuwa zimepungua sana kwa hiyo nikaambiwa nianze dawa za kurefusha maisha mara moja. Tangu nianze kutumia dawa za kurefusha maisha najisikia vizuri. Afya yangu ni nzuri; siumwi umwi tena, nakula vizuri, nafanya mazoezi na nimenenepa kidogo.

Kuambukizwa na VVU siyo kwamba Mungu hakupendi. Wewe siyo mtu mwovu kuliko wengine. Ni kwamba tu umeambukizwa na kwa sasa ni lazima upigane na ugonjwa wako na siyo kusikitika maana kusikitika hakutawaondoa hao VVU mwilini mwako. Huu ni ugonjwa. Ulimwenguni humu kuna magonjwa mengi. Huu ni mojawapo ya magonjwa mabaya na ukiwa nao ujue tu wewe hupo peke yako. Kuna wenzako mamilioni ambao wanateseka kama  wewe. Ukipata VVU siyo kwamba umejamiana ovyo ovyo tu. Kuna ambao wanapata hata bila kujamiana, kuna ambao wanaupata bila hata kutembea nje ya ndoa. Unaweza kupata maambukizi kwa njia nyingi.

Nilimwambia mwajiri wangu kuwa nilikuwa na VVU. Bosi wangu ni mwanamke kama mimi. Alinionea huruma akanipa msaada na nikaendelea kufanya kazi.

Kuwaarifu watu kuwa unaumwa ni jambo zuri lakini chagua wale ambao unaona watakupokea, watakuonea huruma na hawatakutenga. Kama baada ya watu kujua una VVU; wakianza kukutenga, kukunyanyapaa, achana nao. Waache waishi maisha yako na wewe uishi maisha yako.
Mkakati wako ni, “Mpende akupendaye; asiyekupenda; achana naye”

Sasa najiangalia na kuishi maisha yangu siku kwa siku nikimwomba Mungu. Kila ninapoanza siku mpya; kila ninapoamka asubuhi naanza kwa kusali na  kumshukuru Mungu kuwa nimeona siku mpya kwa kuwa najua usiku uliopita wengi wanaougua ugonjwa wangu hawakuona siku hii. Ikifika jioni ninapoingia kitandani kulala namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunilinda siku nzima na kunifikisha usiku wa leo. Najua wengi walio na ugonjwa huu hawakuiona jioni ya leo. Kuna wengi wanaoumwa ugonjwa wangu  na wamekufa asubuhi hii, mchana au jioni hii. Naweka roho yangu mikononi mwa Mungu na kumwomba kama ataamua aniamshe asubuhi, lakini kama sikuamka anipokee kwake baada ya mateso haya hapa ulimwenguni.

Wiki ijayo tutasoma stori ya Aisha ambaye mpenzi wake anayesoma chuo kikuu, inavyoonekana amemwambukiza VVU
Msomaji tuandikie stori yako kama na wewe umeishawahi kuambukizwa au unamjua mtu aliyeambukizwa awe ndugu, rafiki, mfanyakazi mwenzako au jirani. Wataalamu tuandikieni mnavyomwona huyu mama na mnavyoona ugonjwa huu wa hatari: mwandikie Mhariri P. O. Box 72321 Dar es Salaam na bahimokahumba@yahoo.com  simu 0712002188 

Kuugua Saratani

Repoti za mtandao za tarehe 23 Mwezi Februari 2012 zinasema ‘Rais Chavez ana saratani inayohitaji kupasuliwa’


Raisi Hugo Chaves
Raisi Hugo Chavez wa Venezuela alikuwa amelazwa hospitalini huko Cuba  ambapo walimgundua kuwa alikuwa na saratani. Walimpasua na kumtibu kwa kutumia mionzi na baadye alirejea kazini. Baadaye aliporudi tena kupimwa pale walipompasua saratani palionekana bado pana saratani.  Repoti ya wakati huo ilisema kuwa Raisi Chavez  atarudi huko Cuba hapa karibuni kupasuliwa tena na ameisharudi kufuatilia matibabu yake.
Raisi Chavez aliwaambia wananchi wake kuwa ataenda Cuba kwa ajili ya matibabu na wasitegemee kumwona huko nchini kwa wiki chache zijazo. Alisema kuwa pamoja na kuhitaji kupasuliwa atatibiwa kwa kutumia mionzi.
Daktari bingwa wa saratani Mkolumbia  Dr. Carlos Castro alisema kuwa kama Chavez atahitaji kutibiwa kwa mionzi  atahitaji kutibiwa kwa siku 10 kwa hiyo itakuwa lazima amteue msaidizi wake wakati akiwa Cuba kwa matibabu.
Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi huko Venezuela ambapo Chavez ambaye ameishatawala kwa miaka 13 anataka asimame tena aongezewe miaka 6 mingine.

 Chavez mwaka huu wa 2012 ana umri wa miaka 57. Chaves amekataa kata kata uvumi uliokuwa unaenea kuwa alikuwa na saratani ambayoi ilikuwa imeishasambaa na kwa hiyo hawezi tena kazi yake ya Urais na hawezi kusimama tena kugombea Urais. Kama atashindwa kugombea, mshindani wake   Henrique Capriles wa umri wa mika 39 ambaye sasa ni Gavana wa jimbo moja huko Venezuela huenda akashinda kwani inavyoonekana chama cha Chaves hakina mtu mwenye nguvu ya kuwashinda wapinzani.
Chavez alipoenda kutibiwa kwa mionzi aliamua kujinyoa kichwa chake ili kama mionzi ingenyofoa nywele zake basi dalili hiyo haingeonekana sana. Wakati repoti hii ikiandikwa nywele zake zilikuwa zinarudi kuota.

Akiwazungumzia wananchi wake  kwa TV alisema, "Ningependa kuendelea kuishi. Nataka niishi na nyie wananchi wangu, niendelee kupigania maisha bora na nyie mpaka mwisho wa maisha haya yangu alionipa Mungu.”
Madaktari walisema kuwa habari hizi kuwa saratani aliyokuwa nayo imetokea pale pale ilipotolewa saratani, siyo habari nzuri kwa kuwa kama una saratani; baada ya matibabu umehisi umepona na saratani ikitokea pale pale ilipokuwa; siyo jambo zuri; ni jambo ambalo halina matumaini  makubwa. Kama ikitokea pale pale ilipokuwa zamani ni dalili kuwa iliyokuwepo haikupona.
Tarehe 24 February 2012 Chaves alienda Cuba tena kupasuliwa na kutibiwa kwa mionzi. Baadaye mwishoni wa mwezi wa tatu alitokea kwenye TV akiwaambia wanancni wake kuwa alikuwa akiendelea vizuri

Msomaji unaona kuwa saratani ya Rais Chavez siyo tu inatishia maisha yake bali hata kazi zake za Urais. Kama una uzoefu wa jinsi saratani ilivyotishia uhai na maisha yako, ya ndugu, rafiki au mtu yeyote unayemfahamu tuandikie. Tukichapisha uzoefu wako hatutatambulisha jina, anwani au simu kwa kuwa yote haya ni siri yako na mhariri
Tuandikie  mhariri, P.O.Box 72321 Dar es Salaam, bahimokahumba@yahoo.com na 0712002188 au andika kwa hapa chini.


Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana (MYKK)

Tutakuwa tunaelezea kwenye safu hii maambukizi yanayosambazwa kwa kujamiana. Wasomaji wengi wamezoea kuyaita magonjwa ya sinaa lakini gazeti hili linataka tubadilishe tuyaite ‘Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana (MYKK)’ na tutaelezea kwa nini.

 Wanaojua Kizungu labda watakumbuka kuwa hapo awali tulikuwa tunaita hali hizi ‘Sexually Transmitted Diseases (STD). Ukitafsiri moja kwa moja maana yake ni Magonjwa Yanayoambukizwa Kujamiana . Tuliacha kuyaita STD na sasa tunayaita ‘Sexually Transmitted Infections’ (STI) yaani Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana.
Kuna tofauti kati ya magonjwa (diseases) na maambukizi (infections) kwa kuwa magonjwa mengine yanasababishwa na maambukizi. Kwa hiyo tofauti kati ya magonjwa na maambukizi ni kuwa maambukizi yanazaa magonjwa. (Tofauti kati ya yai na kuku ni kwamba kuku anataga  yai).

‘Sexually Transmitted Infection’ (STI)  kwa Kiswahili cha moja kwa moja ni Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana. Sexually transmitted Diseases (STD)  ni Magonjwa Yanayoambukizwa kwa Kujamiana. Utaona kuwa hapa  kuna tofauti kati ya magonjwa (diseases) na maambukizi (infections) Tatizo hapa siyo la ugonjwa tu bali ni la maambukizi. Kunaweza kukawa na maambukizi yanayotokana na  kujamiana ambayo unayaona  maambukizi yenyewe, yaani unaona wadudu ambao mtu ameambukizwa kwa kujamiana, lakini huoni ugonjwa wenyewe. Hii inatokea wa mfano mtu anapoambukizwa na chawa wakati wa kujamiana  (chawa wa mafuzi). Unawaona chawa wenyewe lakini huoni ugonjwa.

Kwenye  tatizo la UKIMWI mtu anaambukizwa  na VVU. Haya ni maambukizi. Ugonjwa hauonekani moja ka moja bali kinachoonekana ni syndroma (dalili nyingi nyingi) inayosababishwa na magonjwa tegemezi yanayouvamia mwili baada ya kinga ya mwili kupungua. Maambukizi mengine kwa mfano ya kisonono na kaswende; ugonjwa unaonekana. Kwa sababu hizi za kuwa kuna hali nyingine ambapo ugonjwa hauonekani moja kwa moja na kwa kuwa katika hali zote kuna maambukizi basi ikakubalika hali hizi ziitwe Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana (Sexually Transimitted Infections - STI)  Magonjwa Yanayosambazwa kwa Kujamiana (Sexually Transimitted  Diseases - STD)

Ni  Maambukizi ya Sinaa (MYS) au ni Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana (MYKK)?
Ni lazima tuwashukuru wataalamu wanaojitahidi kutafsiri maneno yetu ya kisayansi kuyaweka kwenye lugha ya Kiswahili. Tushukuru kuwa tafsiri zao nyingi ni sawa na rahisi kuzitumia lakini kuna tafsiri ambazo wao wametupa kianzio ili na sisi tufikirie tuone kama zinahitaji kuboreshwa. Moja ya tafsiri ambayo inahitaji kuboreshwa ni hii ya kuziita hali hizi magonjwa. Tumeishatoa sababu hapo juu na kuelezea kuwa tuziite hali hizi maambukizi na siyo magonjwa.

Ukimwi unamtesa sana mwathirika
Kwa hiyo tuseme ni Maambukizi ya Sinaa?  Sinaa linamaanyisha starehe. Ni kama tunasema kuwa Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana yanatokana na  sinaa, yanatokana na starehe. Hapa tunakuwa kama tunasema kuwa haya ni maambukizi yanatokana na kustarehe bila hata kusema ni starehe gani - ya kunywa pombe, ya kutumia madawa ya kulevya, ya kucheza dansi na musiki - starehe zipo nyingi. Tuyaite Maambukizi Yanayosambazwa na Starehe ya Kujamiana?

Ni ukweli kuwa ukichukulia kujamiana kama starehe utapata Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana. Yanapotokea kati ya wanandoa yanatokana na mwanandoa mmoja au wote wawili kutokuwa waaminifu na kuchukulia kujamiiana kama starehe.
Ni vizuri jina la hali inayohusiana na ugonjwa unapolisikia linakueleza mengi juu ya hali yenyewe na linakuambia hata namna ya kujikinga na hali hiyo. Hapa ukisikia maneno matatu ya jina la hali hii ‘Maambukizi Yanayoambukizwa kwa  Kujamiana’ tayari umeishajua kuwa haya ni maambukizi; kuwa mwenzako anakuambukiza au wewe unamwambukiza. Ukisikia yanayosambazwa unajua kuwa yanasambazwa na siyo kwamba yanaambukizwa tu. Ukisema yanasambazwa tayari umeishasema kuwa yanaenea haraka sana kutoka mtu  hadi mtu. Ukisikia kuwa maambukizi haya yanatokana na kujamiana unaanza kujisemea ‘nijichunge sana na kujamiana ovyo ovyo.’

Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana (MYKK) ni mtu kwa  mtu;  yaani yanatoka kwa mtu  mmoja yanaenda kwa mtu mwingine.  Siyo kama ilivyo kwenye ugonjwa wa kwa mfano malaria ambao vijidudu hutoka kwa mtu mmoja; vinaingia kwa mbu na baadaye kwa binadamu. Siyo kama wa kichocho ambao vijidudu vinatoka kwa mtu vinaingia kwenye konokono na baadaye vinaingia kwa mtu tena. Wataalamu wanaita hali hii ya jinsi vijidudu vinatoka kwa mwanadamu na baadaye kumrudia tena ‘mzunguko wa maambukizi’ ambapo kuna hatua mbali mbali.

Kwanza kuna wadudu wenyewe kwa mfano wanaosababisha Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana; kuna hifadhi ya hao wadudu kwa mfano hapa anayewahifadhi ni binadamu; halafu wadudu wanaingia kwa mtu mwingine na huyo mtu mwingine anawapeleka tena kwa mtu mwingine. Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana ni ya moja kwa moja kutoka kwa mtu hadi kwa mtu mwingine. Maambukizi ya magonjwa mengine yana mzunguko mrefu zaidi ambapo kuna wadudu wa maambukizi, kuna hifadhi yao ambayo moja inaweza ikawa binadamu (malaria na kichocho) au mnyama (kichaa cha mbwa); wadudu wanatoka kwenye hifadhi wanaingia kwenye mnyama mwingine kama kwa mfano kichocho kinaingia kwenye konokono, kinatoka huko na kuingia kwa binadamu. Kwa kujua mzunguko huu wa vijidudu vya magonjwa inajulikana ni wapi tuingilie ili kuuthibiti ugonjwa wenyewe. Kwa kuwa inajulikana kuwa mzunguko wa Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana ni mtu kwenda kwa mtu; na yanaambukiza kwa kujamiana, kuyakinga haya maambukizi kunahusu kuiangalia hali ya kujamiana na kuhakikisha mtu anajamiana na mwenzake ambaye hana uwezekano wa kuwa na hifadhi ya Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana (MYKK). Kuna watu ambao wana uwezekano zaidi wa kuwa hifadhi ya wadudu wa MYKK.  Kujikinga na maambukizi haya ni vema kutojamiana nao. Hawa ni watu wanaojamiana na watu wengi kwa mfano malaya au hata watu wa kawaida tu mradi wewe mwenyewe umemwangalia na kujua tabia yake. Ukishajua kuwa huyu anajamiana na wanaume au wanawake wengi au zaidi ya mmoja unajua kuna uwezekano kuwa yeye ni hifadhi ya  MYKK.

Tumeelezea ni kwa nini maambukizi haya yaitwe Mambukizi Yanayosambazwa  kwa Kujamiana na siyo Magonjwa Yanayosambazwa wa Kujamiana (STD) au Magonjwa ya Sinaa. Tuyaite Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana au kwa kizungu STI. Wiki ujayo tutataja na kuanza kuelezea aina 13 za MYKK
Tuandikie kama umeishawahi kuugua MYYK utuambie ulivyoambukizwa, ulivyotibiwa na  unavyoendelea. Barua hizi, majina na simu namba ni siri. Mwandike Mhariri, P.O. Box 72321 Dar es Salaam au barua pepe bahimokahumba@yahoo.com, simu meseji 0712002188 au andika kwa hapa chini.

Kuugua Ugonjwa Wa Presha

Ugonjwa wa Presha.

Hunijui Kuwa Niko Mwilini Mwako. Nakutafuna Pole Pole na Mwisho Nitakuangusha.

Tunauongelea ugonjwa wa presha katika gazeti hili kwa sababu zifuatazo: 
  • Ugonjwa wa presha ni ugonjwa unaowaathiri watu wengi, unaowaletea watu wengi matatizo ya kiafya, unajificha mpaka yanapoanza matatizo makubwa, ni mojawapo ya viashiria vya hatari  kinachoungana na viashiria vingine kusababisha mshtuko wa moyo na kiharusi,
  • presha inaviharibu viungo vya mwili kama vile mishipa ya damu, moyo, figo, ubongo na macho; 
  • ni ugonjwa ambao mtu anaweza akauzuia kwa kiasi kikubwa na kama ukishatokea matibabu yake na maendeleo yake hutegemea sana jinsi mgonjwa anavyofanya bidii kuishi staili ya maisha inayohusiana na kushuka na kuthibiti presha yake.
  • Tutaelezea maana ya presha kwenye damu, namna ya kupima presha ya damu, maana ya ugonjwa wa presha, ni nini kinachousababisha, dalili zake, matatizo yake na unavyohusiana na staili za maisha. Makala ya leo tutaelezea maana ya presha yaani shinikizo au msukumo wa damu na kuelezea daktari anavyopima presha.

Nini maana ya presha ya damu?



Neno la Kizungu ni ‘pressure’ (presha) au kwa Kiswahili shinikizo. Shinikizo la damu au presha ni hali ya msukumo iliyomo kwenye damu.  Kinachofanya damu itembee na kuzunguka mwilini ni presha yaani msukumo wa damu.
Presha ni nguvu ya msukumo au nguvu ya kusukuma. Mfano mzuri wa kuelezea maana ya presha ni huu wa presha ya maji ya bomba. Kinachofanya maji yafike nyumbani kwetu ni presha, ni msukumo wa maji. Kwa mfano huku kwetu Mbezi, asubuhi maji yanatoka kwa presha kubwa sana. Ikifika saa 4 hivi presha inapungua na ikifika saa 7 hakuna presha ya maji kabisa na maji hayatoki mpaka kesho yake asubuhi yatakapotoka tena kwa presha kubwa sana.
Kuna njia nyingi za kujua kuwa damu ina presha, ina msukumo au shinikizo. Damu ina presha tukimaanisha inatoka kwa msukumo. Presha ni nguvu ya msukumo au nguvu ya kusukuma. Ukijikata mshipa wa damu ambao ni mkubwa damu inatoka kwa presha, kwa msukumo mkubwa, kwa shinikizo.
Makabila wanaotumia damu kama chakula wana njia ya kupata damu kutoka kwa mnyama (ng’ombe) ili kupata damu ya kumtengenezea chakula mama aliyejifungua. Wao wanajua kuwa mama anahitaji chakula chenye damu ili naye ajitengenezee damu mwilini ili kumrudishia damu aliyotumia wakati wa mimba na aliyopoteza wakati wa kujifungua. Wazee wachungaji wanajua mshipa wa damu ambao wakiutoboa hutoa damu kwa presha, kwa msukumo, kwa shinikizo na kupata damu ya kutosha.


Moyo unapampu damu mwilini

Daktari anapofanya operesheni kubwa kwa mfano ya tumbo hukata mishipa ambayo mara ikikatwa tu unaona damu inatoka kwa presha, kwa msukumo, kwa shinikizo. Anachofanya msaidizi wake ni kuweka ‘presha’ juu ya mshipa uliokatwa na kuzuia usitoe damu zaidi na huko daktari akitayarisha uzi wa kufunga huo mshipa.

Mfano mzuri zaidi wa kujua kuwa damu ina presha, ina shinikizo au msukumo ni unapomwona mtu anatoa damu ya kuwasaidia wagonjwa au kama wewe mwenyewe umeishawahi kutoa damu. Sindano inawekwa kwenye mshipa na hapo mara unaona damu inaingia kwenye mpira ulioungana na hiyo sindano na kumiminikia kwenye chupa. Presha, shinikizo au msukumo wa damu unaisukuma damu iende kwenye chupa na baada ya muda kidogo unaona presha, msukumo wa damu, shinikizo la damu limeishasukuma damu kutoka kwa Msamaria mwema na ameishatoa nusu lita ya damu yake kuwasaidia wagonjwa.

Presha ya damu inaisukuma damu painti moja hii kutoka kwa msamaria mwema kumpa mgonjwa
Presha ni mojawapo ya vipimo nyeti ambavyo hutumika kufuatilia (monitor) hali ya  mgonjwa. Vipimo vingine nyeti ni hali ya joto mwilini (temperature),  kupumua na  mapigo ya moyo (palsi). Presha huwa inabadilika badilika kutegemea na kama umelala, umekula, unafanya mazoezi, ni mgonjwa, una msongamano wa mawazo (stress), umesimama au umelala nakadhalika. Presha vile vile inapanda jinsi umri unavyosogea.
Presha ina namba mbili: ya juu na ya chini.  Ya juu ni wakati vyumba vikubwa vya moyo (vyumba vya chini) vinapopampu damu na kuielekeza mwilini. Ya chini  ni wakati moyo unapotulia kabla haujaendelea kupampu. Hii ni presha iliyopo wakati wa katikati ya mapigo ya moyo. Kwa kuwa kipindi hicho wakati moyo unapampu damu kinaitwa kwa kitaalamu ‘systole’ na kipindi hicho wakati unapojilegeza kabla ya kupampu tena ‘diastole’ presha hizi mbili zinaitwa ‘systolic’(sis-tolik) na ‘diatolic (daya-stolik). Kwa hiyo presha inaripotiwa ya juu (systolic) na ya chini (diastolic) kama 120/80 (120 kwa 80). Mgonjwa atakuambia, “Nimepimwa presha na nimeambiwa ni 120 kwa 80 yaani ‘systolic’ ilikuwa 120 na ‘diastolic’ ilikuwa 80”
Ni matumaini yangu kuwa umeelewa maana ya presha na kuwa presha ina tarakimu mbili moja ikiitwa ‘systole’ na nyingine ‘diastole’. Wiki ijayo tutaelezea namna ya kupima presha.

Maoni na maswali mpelekee mhariri P.O.Box  72321 Dar es Salaamu, bahimokahumba@yahoo.com na 0712002188 au andika hapa chini.


Kuugua Kisukari

Hunijui kuwa niko mwilini mwako. nakutafuna pole pole. Na mwisho nitakuangusha !


Ugonjwa wa Kisukari - Dr. Tengio Urrio


Ugonjwa wa kisukari ni ugonjwa wa mwili kushindwa kuthibiti na kurekebisha kiasi cha sukari mwilini.
Leo tutaanza makala ya kwanza kati ya makala zaidi ya 30 ya kuelezea juu ya ugonjwa wa kisukari. Tutaanza kwa kuelezea kisukari ni ugonjwa gani na kwa kuwa unahusu homoni ya insulini inayotengenezwa na glandi ya pankrasi tutaanzia kwa kuelezea maana ya systima za mwili, homoni ya insulini na glandi ya pankrasi. Baadaye tutazungumzia kisukari ni nini, dalili zake, matatizo yake na matibabu yake. Tutazungumzia vile vile matatizo ya mama mjamzito wakati ana kisukari.
Tuanze makala ya kwanza kwa kusema kuwa wanafunzi wanaojifunza kuwa madaktari huanza kwa kujifunza masomo manne makubwa: anatomia (Anatomy), fisiologia (physiology), bayokemia ( biochemistry) na pathologia (pathology). La kwanza,  anatomia ni somo la kufahamu muundo wa kila sehemu ya mwili wa mtu, la pili (bayokemia)  na la tatu (fisiologia)  ni kujua jinsi mwili unavyofanya kazi. Hujifunza, kwa mfano,  namna mwili unavyomeng’enya na kuchanganya vyakula na hewa ili kuzalisha nishati ya kuendesha mwili. Katika somo la patholojia wanajifunza mabadiliko yanayotokea kwenye sehemu za mwili wakati zinapoingiliwa na magonjwa.  Masomo haya manne ndiyo misingi ya kujifunza na kuelewa juu ya ugonjwa wowote pamoja na ugonjwa wa kisukari. Kwa mfano, ukitaka kuelezea juu ya ugonjwa wa kisukari huna budi kuongelea juu ya anatomia na patholojia ya kiungo kinachotengeneza homoni inayohusika kwenye ugonjwa wa kisukari. Ukitaka kuelezea kisukari kinavyodhuru jicho huna budi kuongea juu ya anatomia ya jicho.
Ili kuuelewa ugonjwa wa kisukari, hatuna budi kuyapitia masomo haya manne kwa angalau kiasi kidogo kila inapobidi.

Makundi ya magonjwa
Magonjwa yanaweza yakagawanyika kwenye makundi mawili muhimu: yanayoambukizwa na yasiyoambukizwa. Magonjwa yanayoambukizwa ni kama malaria,  VVU, kisonono, safura, TB, kichocho, kichomi, kifua kikuu nakadhalika. Kundi la pili, yaani magonjwa yasiyoambukizwa lina magonjwa kama ugonjwa wa presha, kisukari, saratani na magonjwa ya moyo. Ugonjwa wa kisukari ndio ugonjwa wenye wagonjwa wengi zaidi katika kundi hili la magonjwa yasiyoambukizwa. Kuna watu karibu milioni mia moja wenye kisukari ulimwenguni. Kwa hiyo kama wewe una ugonjwa wa kisukari fahamu tu kwamba haupo peke yako kwani kuna wenzako milioni mia moja wenye ugonjwa kama wa kwako.
Kipimo cha sukari

Systima za mwili
Mwili umejengwa na vitofali vidogo vidogo vinavyoitwa seli. Mkusanyiko wa seli za aina mbali mbali zinazoshirikiana katika kufanya shughuli moja au shughuli mbali mbali unaitwa tishu na tishu mbali mbali zikikusanyika na kushirikiana kufanya kazi moja au zaidi; mkusanyiko huu unaitwa kiungo. Mwili una viungo vingi kama ini, figo, ubongo, pankrasi nakadhalika.  
Kiungo kinachohusika kwenye ugonjwa wa kisukari kinaitwa pankrasi. Kwenye kiungo hiki kuna seli na tishu mbali mbali. Selli zinazohusika na ugonjwa wa kisukari ni zile zinazotengeneza homoni ya insulini.
Viungo mwilini vinaungana na kuwa na systima ambayo ni mkusanyiko wa viungo vikiungana na kufanya shughuli moja au zaidi. Mwilini kuna systima 13  ambazo ni:  systima ya ubongo na neva; moyo, damu na mishipa ya damu; kupumua; kumeng’enya chakula; kinga; musuli; mifupa; kutoa taka; homoni; ngozi, uzazi na sensi

Glandi ni nini?
Kuna viungo mbali mbali mwilini moja ikiwa ni kundi ambalo linaitwa ‘glands.’ Hii ni mojawapo ya sehemu ya mwili wetu ambayo bado sijaweza kupata neno lake la Kiswahili. Kwa sasa tutafsiri neno la kitaalamu ‘glands’ kama glandi kwa Kiswahili. La maana ni kujua kuwa tunazungumzia nini tukisema mwilini kuna glandi. Mfano wa glandi ni kama zile zinazotoa machozi na zinazotoa mate. Tezi vile vile ni aina ya glandi. Kazi za glandi ni kutengeneza vimeng’enyo na homoni. Ziwa ni glandi maana hutengeneza maziwa na kuyaingiza kwenye mrija na kumpelekea mtoto anyonye kwenye chuchu ya ziwa.
Kuna aina mbili za glandi. Moja ni zile ambazo zikishatengeneza vimeng’enyo huviweka au huvifikisha kwenye mrija ambao utavipeleka huko vinakohitajika. Ya pili ni pale glandi haina mrija. Kimmeng’enyo au homoni inayotengenezwa humo huingia moja kwa moja kwenye damu. Glandi muhimu inayohusika kwenye ugonjwa wa kisukari ni pankrasi. Glandi hii inatengeneza homoni inayoitwa insulini.

 
Homoni ni nini?
Systima ya homoni ni mojawapo ya systima za mwili. Systima hii ni mkusanyiko wa glandi; kila moja ikitengeneza homoni muhimu za kuendesha, kurekebisha au kuthibiti shughuli maalumu kwenye mwili. Homoni ni kemikali zinazotengenezwa na viungo vya systima ya homoni. Homoni zikishatengenezwa huingia moja kwa moja kwenye damu na kupelekwa kwenye viungo lengwa zinapohitajika kuendesha, kuthibiti au kurekebisha shughuli kwenye viungo lengwa.
Mwilini kuna zaidi ya homoni 50. Kwa hiyo magonjwa yanayotokana na systima ya homoni ni mengi. Moja ya magonjwa kwenye systima ya homoni ni ugonjwa wa kisukari. Homoni inayohusika kwenye ugonjwa wa kisukari ni homoni inayoitwa insulini ambayo inatengenezwa na kiungo kinachoitwa pankrasi. 
Turudie kwa kutia msisitizo kuwa moja ya systima kumi na tatu za mwili ni systima ya homoni. Humo kwenye systima ya homoni kuna glandi ambazo ni viungo vinavyotengeneza homoni. Homoni ni kemikali zinazotengenezwa na glandi na kuingia moja kwa moja kwenye damu na kupelekwa kwenye viungo lengwa zinapohitajika kuendesha, kuthibiti au kurekebisha shughuli kwenye viungo hivyo. Homoni inayohusika na ugonjwa wa kisukari inaitwa insulini na inatengenezwa na glandi inayoitwa pankrasi.

Wiki ijayo tutaelezea juu ya kiungo hiki cha pankrasi na kuelezea kinafanya kazi gani,


Kidonda kwenye mguu mgonjwa wa kisukari
Wasomaji tunaomba maswali na maoni yenu kuhusu ugonjwa wa kisukari. Wataalamu tunaomba mawazo na maoni yenu mwandikieni Mhariri P.O. Box 72321 Dar es Salaam,  Au changia maoni yako hapa chini.