Watu wanaowapiga wake zao
Nini maana ya Ukatili Kijinsia (UWAKI)?
Ukatili wa kijinsia au UWAKI ni ukiukwaji wa haki za binadamu ambapo mtu kwa kutumia maungo, hisia za kujamiana au kujamiana, au hisia za akili na kisaikolojia anamsababishia madhara mtu mwingine kwa kuwa yeye yeye mtuhumiwa anayesababisha madhara, anajisikia au anaamini kuwa ana uwezo na mamlaka juu ya mwathirika yaani huyo anayemthuru.
UWAKI hujumuisha vitendo anavyofanyiwa mwanamke au mwanamme (mwathirika) bila ridhaa yake kutokana na mwanamme au mwanamke anayevifanya (mhalifu) kufikiria kuwa ana madaraka dhidi ya mwathirika.
Ukatili wa Kijinsia ni pamoja na kujamiana bila ridhaa ya mwathirika kihisia na kwa kutumia viungo vya siri, ukatili wa kimwili na wa kisaikojia, kufanya vitendo vya jadi vyenye madhara kama kukekeketa wasichana na wanawake na ukatili wa kiuchumi na wa kijamii.
Ukatili huu unawalenga watu kwa misingi ya kijinsia kwamba wao ni wanawake au ni wanaume basi wanafanyiwa vitendo hivyo.
Ukatili wa Kijinsia ni ukatili unaotokea kati ya wanaume na wanawake ambapo kawaida anayefanyiwa ukatili ni mwanamke. Ukatili huu unatokana na kutokuwa na uwiano wa mamlaka walio nao watu wa jinsia ya kike na ya kiume, wanaume wakionekana au wakifikiri kuwa wana mamlaka zaidi dhidi ya wanawake na hata wanawake nao wakifikiri kuwa wanaume wana mamlaka zaidi kuliko wao. Wanawake ndio hasa wanaofanyiwa ukatili kwa kuwa tu ni wanawake kwa hiyo pamoja na kuwa ukatili wa kijinsia unahusisha jinsia zote mbili, akina mama ndio hasa wanaoadhirika zaidi. Ukatili wa kijinsia ni pamoja na kutumia maungo, ukatili unaohusu kujamiana na unaohusu kuathirika kiakili.
Akina mama wengi na akina baba wachache wanateseka sana kimya kimya katika ndoa au mahusiano kutokana na kufanyiwa vitendo vya UWAKI. Aina za ukatili wa kijinsia ni kufanya ukatili kutumia maungo, ukatili unaohusu kujamiana, unaohusu mateso ya kiakili, unaotokea kwenye familia, ukatili kwa watoto, ubakaji, ubakaji unaotokea kwenye mahusiano ya ndoa, unyanyasaji wa kijinsia pahala pa kazi, mashuleni na kwenye vyuo; kuingizwa kwenye shughuli za umalaya kwa nguvu, kusafirishwa kwenda kufanyishwa kazi au umalaya na kukeketwa kwa wasichana na akina mama.
Ijapokuwa tunasema kuwa akina mama na wasichana ndio hasa wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia ukweli ni kuwa hata wanaume na vijana wa kiume wanafanyiwa ukatili wa kijinsia.
Taarifa juu ya unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa majumbani, ubakaji ndani ya ndoa na ndoa za wasichana wadogo, bado ni tatizo kubwa hapa Tanzania. Ukeketaji wa wasichana unaendelea kama kazi yaani ni mazoea, ikiwa ni pamoja na hata kwenye baadhi ya maeneo ya mijini.
Kuna ripoti na mashtaka machache sana ya waathirika wa Ukatili wa Kijinsia (UWAKI) wakiwashtaki waliowafanyia ukatili. Kati ya kesi hizi ni chache sana zinafika mahakamani na hata zile zinazofika mahakamani ni chache sana zinafikia kutolewa hukumu
Kuna ripoti na mashtaka machache sana ya waathirika wa Ukatili wa Kijinsia (UWAKI) wakiwashtaki waliowafanyia ukatili. Kati ya kesi hizi ni chache sana zinafika mahakamani na hata zile zinazofika mahakamani ni chache sana zinafikia kutolewa hukumu
Wasomaji tuandikieni mawazo yenu na uzoefu wenu juu ya unyanyasaji wa kijinsia. Wewe mwenyewe au jirani au ndugu yako amenyanyaswa au kufanyiwa ukatili wa kijinsia? Mwandikie mhariri, P.O.Box 72321 Dar es Salaam au e mail bahimokahumba@yahoo.com au sms 0712002188
Washikaji:
Mshikaji 1: Jana jirani yangu alitusumbua sana kwa makelele usiku. Mwanamme alikuwa analia kwa nguvu “Ntakuua! Ntakunyonga! ntakumaliza!” na huko tunasikia mangumi Pa! Pa! Pa! Pa!
Mshikaji 2: Ndio ilivyo; sisi akina baba wakati mwingine ni wakatili. Tunawadunda sana wake zetu. Siku moja nao watatudunda.
Mshikaji 1: Kwani aliyekuwa anadundwa ni mke basi. Tulipokimbilia nyumbani kwao tulimkuta mke amemwangusha mme wake na amemkalia tumboni; anamdunda sawa sawa. Kumbe mwanamme kwa kulia kule alikuwa anaomba msaada lakini hakutaka majirani tujue kuwa aliyekuwa anadundwa ni yeye mwanamme.
Ameneh Bahrami sasa ni kipofu
Huko Iran mwaka wa 2004 baba mmoja alimwagia tindi kali dada mmoja kwa kuwa eti alikataa awe mchumba wake; alimkatalia penzi kwa hiyo akamwagia tindikali machoni na kumsababishia majeraha usoni na upofu.
Huu ndio ukatili kweli kweli. Ni UWAKI kwa kuwa huyu baba kafanya hivyo kwa kuwa ana hisia kuwa eti kwa kuwa ni mwanamme basi ana pawa (power) kuliko wanawake na mwanamke hawezi akamkatalia penzi. Kwa kuwa yeye ni mwanamme basi akimtongoza mwanamke basi ni lazima huyo mwanamke amkubalie.
Baada ya kumwagia tindikali na kumsabaishia makovu usoni na upofu, mahakama ya huko Irani iliamua kuwa kwa kuwa sheria za nchi hiyo zina misingi ya jino kwa jino basi huyu baba amwagiliwe naye tindi kali usoni kwenye macho naye apofuke. Waliamuru kuwa aende hospitali na huyu mama akishirikiana na daktari wamwekee tindi kali machoni. Adhabu hiyo ilikuwa itekelezwe mwezi wa saba mwaka wa 2011. Baba alipelekwa hospitalini na daktari akajiweka tayari kumdondoshea matone ya tindi kali kwenye macho. Mara akafika yule mama na kusema kuwa anamsamehe!
Mama huyu mwenye huruma alikuwa amesindikizwa hospitalini humo na ndugu zake wawili wakimshikia kulia na kushoto. Akionekana na makovu yake usoni na machoni na kwenye mdomo; alionekana kuwa ni mama mwenye maumivu makubwa rohoni lakini alikuwa na moyo wa huruma. Alimsamehe mbaya wake aliyemsababishia vilema vya maisha usoni na upofu.
Mama huyu anayeitwa Ameneh Bahrami alisema, “Ni vema mtu usamehe, sitaki kulipiza kisasi.’ Mbaya wake Majid Movahedi alipiga magoti na kushukuru akilia huko akiushikilia ukuta.
Sheria ya jino kwa jino inayojulikana kwa jina la ‘qisas’ (kisas) inasema kuwa pale mtu ameleta majanga basi familia yake au yeye mwenyewe huomba radhi; humwomba aliyedhurika asamehe na kukubaliana fidia bila hivyo sheria ya jino kwa jino ichukue mkondo wake. Kwa hali hiyo mwaka wa 2010 jamaa mmoja ilibidi akatwe mkono wake kwa kuwa alitenda kosa ambalo aliyemtendea hakukubali asamehewe.
Huyu mama ambaye sasa ana vilema vya maisha, baada ya msamaha huo; huyu baba itabidi akae gerezani mpaka mahakama itakapoamua apewe adhabu gani nyingine ambayo ni pamoja na kumfidia huyu mama aliyekuwa kipofu na uso wake kuharibika.
Shirika la Haki za Binadamu (Amnesty International) wanaipinga sheria hii ya Iran ambayo inampa mtu adhabu ya kutegemea na kosa alilofanya. Kama amemfanya mtu kipofu basi naye apofuliwe. Kama amemkata mtu mkono naye akatwe mkono. Kama ameua naye auawe. Kama jicho likiharibiwa kwa kuwa alimwagia huyu mama tindi kali, basi na yeye amwagiliwe tindi kali machoni asikie maumivu makali kama aliyomsababishia aliyemjeruhi. Shirika la ‘Amnesty International’ linasema eti pamoja na kwamba mtu amefanya kitendo cha ukatili siyo vizuri naye kumfanyia mbaya wake ukatili. Kitendo cha kinyama kikifanyika na kumjeruhi mtu ni kwamba kimeishafanyika. Kumfanyia unyama aliyekifanya hicho kitendo inakuwa ni unyama mkubwa zaidi. Siyo sawa kumfania vibaya mtu aliyefanya ubaya eti kwa kulipiza kisasi!
Msomaji hili linakuingia kichwani? na wewe unasemaje na hili? Mwandikie mhariri P.O.Box 72321 au bahimokahumba@yahoo.com Dar es Salaam au sms 0721002188 au andika hapa chini.
No comments:
Post a Comment