Kifo cha Ujanani. Amy Winehouse- Nyumba ya Mvinyo
(miaka 27) Kanumba (Miaka 28)
Huko Ulaya mwaka jana tarehe 22 na 23 Juy 2011 kulitokea matukio mawili ya kihistoria na ya kusikitisha. Huko Norway tarehe 22 July 2011 kijana mmoja wa miaka 32 aliua watu 7 na kujeruhi wengine 95 kwa kuweka bomu kubwa kwenye jumba la ghorofa lenye ofisi za serekali. Baada ya kuweka bomu hilo kwenye nyumba hiyo na wakati akingoja lilipuke alienda kwenye kisiwa kimoja ambapo vijana walikuwa wamekusanyika kwenye mkutano akaanza kuwamiminyia risasi. Wengi wa hawa vijana walikimbilia baharini na wakati wakijitahidi kuogelea aliendelea kuwamiminia risasi wakiwa humo baharini. Ilikuwa ni gharika, ni kiama, ni jambo la kusikitisha jinsi mtu huyu kijana wa miaka 32 alivyoamua kuua vijana wenzake na watu wengi waliokuwa kwenye hilo jumba la serekali.
Kesho yake huko Uingereza ambapo wiki hiyo habari kubwa iliyotokea ni kuwa mtu mmoja maarufu mwenye magazeti mazito ya ‘News of the World’ wandishi wake walikuwa na majambo ya kihuni ya kuingilia simu za watu na kusikiliza mazungumzo yao. Walikuwa na nguvu hizo kiasi kuwa waliweza hata kuitega simu ya Waziri Mkuu wa Uingereza na kusikiliza mambo yake ya kisiri.
Siku hiyo ya terehe 23 mwezi wa July 2011 kilitokea kifo cha msichana wa miaka 27 aliyezaliwa siyo zamani sana ila juzi juzi tu mwaka wa 1983 na siku hiyo mwaka huo wa 2011 alikuwa maiti. Ilihisiwa kuwa kifo chake kilitokana na matumizi ya pombe na madawa ya kulevya. Haikujulikana usiku huo alipofariki kama kifo chake kilitokana na kujiua au kutumia dozi kubwa mno ya madawa hayo na pombe.
Dada huyu mwenye sauti nzuri ambaye alikuwa amepata tuzo la ‘granny award’ alikuwa ameenda kwenye kambi ya kutibu ugonjwa huo wa matumizi ya pombe na madawa ya kulevya yaani ‘rehab’ kwa kizungu. Ilivyoonekana alitoka huko kabla hajapona vizuri. Kama mtu akianza kutumia madawa ya kulevya akishaenda kambini huko kutibiwa, huwa anakaa kwa mda mrefu. Lakini kwa wasanii na watu ambao wako ‘bisy ‘na ambao wamezungukwa na watu na wafanyakazi ambao kula kwao ni kutokana na kazi za msanii; huyo msanii asipoonekana hadharani kwa mda mrefu eti yuko kwenye jumba la kutibu madawa ya kulevya humshindikiza atoke humo. Kula kwao ni kutokana na huyo msanii kwa hiyo humhimiza atoke haraka huko wakimwambia, “Wewe vipi; toka huko ‘rehab’ tukatafute pesa. Unadhani sisi tutakula wapi? Tukale Polisi?”
Inavyoonekana huyu msichana Amy Winehouse alitoka mapema huko kwenye ‘rehab’ na alipotoka hakuwa amepona vizuri na akaishia baadaye siku hiyo ya terehe 23 mwezi July 2011 aidha kujiua au kwa makosa kutumia dozi kubwa ya pombe na madawa ya kulevya. Alikufa kabisa, masikini kutokana na pombe na madawa ya kulevya. Alivyosema mshabiki mmoja ‘Taa iliyowaka kwa mwanga mkubwa imezimika mapema, na mapema sana’
Jina lake la pili Amy ni ‘Winehouse’ maana yake nyumba ya mvinyo. Mwili wake ulikuwa ni nyumba ya mvinyo lakini ikawa nyumba ya pombe na madawa ya kulevya. Nyumba ya pombe na madawa ya kulevya haiishi kwa mda mrefu. Ilibomoka na kuishia mapema. Mungu ailaze roho yake penye upepo mwanana.
Msanii mwingine ambaye ni mshumaa uliomulika kwa mda mfupi ni Steven Kanumba, mcheza filamu maarufu wa Tanzania ambaye alifariki usiku wa Ijumaa kuu mwaka huu na kuzikwa Jumanne ya tarehe 12 April 2012. Kanumba alizaliwa January 1984 na kufa April 2012 akiwa na umri wa mika 28 karibu sana na umri wa Amy aliyefariki akiwa na umri wa miaka 27. Kwa neema yake Mwinyezi Mungu, Mwingi wa Rehema wasanii hawa wapumzike kwa Amani’
Steven Kanumba ‘mshumaa uliowaka kwa mda mfupi.’
|
No comments:
Post a Comment