Watu Wasio na Rangi ya Ngozi, Macho na Nywele!
Tarehe 4 May ni siku ya Albino duniani. Siku ya albino duniani ni siku tunayotumia kuendeleza kuhamasisha juu ya kuelewa zaidi kuwepo kwa wenzetu wasio na rangi ya ngozi, macho na nywele na jinsi ya kushirikiana nao kuyatatua matatizo yanayoambatana na hali hii.
Baada ya siku ya albino duniani, gazeti hili linaendelea kuhamasisha ushirikiano wa kila mmoja wetu kufahamu juu ya hali hii, matatizo walio nayo walio na hali hii na kushirikiana nao katika kuyatatua. Tuongee juu ya hali hii muhimu, ‘Kutokuwa na Rangi ya Mwili, Macho na Nywele’.
Katika kushirikiana na wenzetu wasiokuwa na rangi ya ngozi macho na nywele ni muhimu tuipe hali hii jina linaloeleweka. Makala ya leo ni kuelezea ni kwa nini tuache kuiita hali hii albino, ulemavu wa ngozi, ulemavu wa rangi ya ngozi na badili yake tuiite ‘ Watu Wasio na Rangi ya Ngozi, Macho na Nywele.’
Sisi hatuna rangi ya ngozi lakini wote tu binadamu wa Mungu Mmoja Chini ya Jua Moja, Mwezi Mmoja na Mamilioni ya Nyota
|
Tuwaite albino?
Wanadamu wasio na rangi ya asili (melanin) tunawaita albino ambalo ni jina la Kiyunani linalomaanisha rangi. Jina hili halielezi ya kutosha hali hii kwani kusema tu albino yaani rangi haitoi maana yeyote. Hata hivyo kwa sababu tumeishawahi kulisikia mara nyingi na tumewaona albino, mtu akilisema tunajua anachosema. Lakini akilisikia mtu ambaye hajawahi kuwaona albino au mtoto mdogo kwa mara ya kwanza hana budi kuuliza maswali mengi kabla ya kuelewa hali yenyewe au watu wenyewe.
Tuwaite wenye ulemavu wa ngozi?
Jina lingine tunalosikia ni ‘ulemavu wa ngozi’ lakini kwa sababu kuna aina nyingi za ulemavu wa ngozi kusema tu ni ulemavu wa ngozi haitoshi na hata hivyo kama ni ulemavu siyo tu wa ngozi bali ni wa macho na nywele kwani hali hii inaonekana kwenye ngozi, nywele na macho. Lakini pia sioni ni kwa nini tunasisitiza sana kuwa ni walemavu kwani neno hili linaleta siyo tu unyanyapaa bali hata wao kujisikia, ‘Sisi niwalemavu, jamii inasema kuwa sisi ni walemavu’.
Tuwaite wenye ulemavu wa rangi ya ngozi?
Jina lingine tunalosikia ni ‘ulemavu wa rangi ya ngozi.’ Hapa kuna tatizo la kuwa jina hili linasisitiza sana kuwa hali hii ni ya ulemavu kiasi cha kuwafanya wahusika wajisikie ‘sisi ni walemavu.’ Hakuna sababu ya kusisitiza kuwa huu ni ulemavu kwani kwa mfano katika hali nyingine za kurithi hatukutaja kuwa zinaitwa ulemavu. Kwa mfano ugonjwa wa ‘siko selli’ ambapo mwili badala ya kuwa na haemoglobin (HB) ya kawaida inakuwa na HB tofauti, hatukuiita hali hiyo ulemavu wa damu. Kama ni kutumia neno ulemavu hapa hilo nenno lingrstahilizaidi kwa kuwa ukwelini kuwa hiyo HB ipo na iliyopo hiyo ina ulemavu. Lakini kwa ndugu zetu wasio narangi ya ngozi; ni kwamba hiyo rangi haipo kabisa. Sasa unawezaje kusema kitu ni kilemavu wakati hakipo. Kunatofauti ya kuwa na maji machafu na kutokuwa na maji kabisa. Utasema sisi tunamaji lakini ni machafu. Utasema sisi hatuna maji. Kwa hiyo tatizo hapa siyo ulemavu wa rangi ya ngozi. Tatizo ni kuwa hiyo rangi haipo kabisa.
La maana hapa ni kutafuta jina ambalo halisisitizi kuwa ni ulemavu na ambalo linaielezea moja kwa moja hali yenyewe ili mtu bila hata kusoma makala marefu kama hii aelewe hali tunayozungumzia.
Wanadamu kwa kirangi wako aina tatu: wenye rangi nyingi (Waafrika) wenye rangi ya ngozi kidogo (Wazungu) na wasio na rangi. Kwa hiyo huoni kuwa jina sahihi la hali hii ni ‘Watu Wasio na Rangi ya Ngozi, Macho na Nywele’ (WWRNMN). Kwa kuwa hili ni jina refu na hali hii ya kutokuwa na rangi ya ngozi inajulikana kuwa inaambatana na kutokuwa na rangi kwenye macho na nywele tungeweza tukaacha macho na nywele na kusema tu ‘Watu Wasio na Rangi ya Ngozi’ kwa kujua kuwa yeyote anayetusikia ataelewa au tutamwelewesha kuwa pamoja na kutokuwa na rangi ya ngozi, mhusika vile vile hana rangi kwenye macho na kwenye nywele. Ili kuelewa zaidi ni kwa nini tusiwaite ‘walemavu’ bali tuwaite ni ‘Watu Wasio na Rangi ya Ngozi, Macho na Nywele’ tueleze maana ya ‘ulemavu.’
Ulemavu ni nini?
Maneno yanayohusiana na ulemavu ni maneno mawili yaani udhaifu na upungufu. Mtu anapokuwa na ulemavu anakuwa na udhaifu au upungufu fulani. Kiungo cha mwili au shughuli fulani ya mwili inakuwa imeharibika au imedhoofika. Mtu anakuwa hawezi kabisa au uwezo umepungua wa kufanya kitu fulani au shughuli fulani ambayo sasa ina kikomo, ina mipaka, ina udhaifu na mapungufu. Mtu anapata matatizo ya kushiriki katika shughuli fulani. Kushiriki kwake kunakuwa na kizuizi na mipaka.
Udhaifu au mapungufu haya yapo ya aina mbili yaani ya kurithi yaani mtu anazaliwa nayo na yanayotokea baada ya kuzaliwa. Tunaweza tukaweka ulemavu katika makundi matano: ulemavu wa viungo; wa sensi za mwili (kuona, kusikia, kugusa, kuonja kwa ulimi); ulemavu wa ufahamu; wa akili na wa kutokana na magonjwa yaliyo kroniki. Mtu anaweza akawa na ulemavu unaoweza kuingia katika makundi zaidi ya moja na hata yote matano. Anaweza kwa mfano kuwa na ulemavu wa viungo na hapo hapo akawa na ulemavu wa sensi za mwili, ufahamu, wa akili na utokanao na ugonjwa ambao ni kroniki.
Sasa tuangalie WWRNMN wana ulemavu gani katika haya makundi matano ya ulemavu ambao unastahili kuwaita walemavu au wenye ulemavu. Wana ulemavu wa viungo? Nafikiri jibu ni ndio maana ngozi ni kiungo. Hiki kiungo hakina rangi kwa hiyo tukubali kuwa kina ulemavu pamoja na kuwa tulikataa hapo juu kusisitiza kuwa ngozi ina ulemavu. Pia wana ulemavu wa macho kwani hawaoni vizuri. Lakini bado nasisitiza kuwa, pamoja na ulemavu huu wa ngozi na macho, kuwaita walemavu wa ngozi tunasisitiza bila sababu ya msingi kuwa ni walemavu. Wana ulemavu wa sensi za mwili (sensory) kama kuona, kusikia nakadhalika? Ndio wana ulemavu wa macho na wachache wana ulemavu wa masikio lakini tunasema hata hivyo hilo halisababishi sisi kusisitiza kuwa ni walemavu. Ni ulemavu unaohitaji kupimwa na kurekebishwa kwa kutumia vifaa kama miwani ya jua, kuvaa kofia kubwa na kutumia miwani. Hatusemi kuwa haya siyo vilema lakini pamoja na kwamba ni matatizo yanayoambatana na hali hii hayatoshelezi kama sababu ya kuita hali hii ulemavu. Wana ulemavu wa ufahamu? Hapana. Wana ulemavu wa akili au wa kutokana na magonjwa ya gafla kama polio au ya kroniki? Hapana..
Kwa sababu tatizo la hali hii siyo ulemavu bali ni kutokuwepo kwa rangi ya ngozi, nywele na macho nafikiri msomaji utaona hakuna haja kuwaita ‘Wenye Ulemavu wa Ngozi’ Ukweli wao ni ‘Watu Wasio na Rangi ya Ngozi, Macho na Nywele.’ Na ni vema wao wasijisikie kuwa wana ulemavu na jamii isiwaone kama watu wenye ulemavu. Ndio jamii iwaone kama watu wenye mahitaji ya kipekee lakini wasisitize kuwa ni walemavu. Tunahitaji kuelimisha zaidi juu ya hali hii hasa kutokana mauaji ya hawa ndugu Wasio na Rangi ya Ngozi, Nywele na Macho.
Tangu mwaka wa 2007 watu wanaoishi na ulemavu wa ngozi 74 wameumizwa vibaya na kati yao 62 waliuawa na 12 wakabaki na madonda mabaya
Wasomaji, wataalamu na Wasio na Rangi ya Ngozi, Macho na Nywele tupeni maswali na maoni yenu. Mwandikie Mhariri P.O Box 72321 Dar es Salaam au e mail bahimokahumba@yahoo.com au meseji 0712 002188 au andika kwa hapa chini.
No comments:
Post a Comment