Wednesday, July 25, 2012

Utoaji mimba

Turuhusu Utoaji mimba?
Katika makala haya tunajaribu kuwaasa wasomaji waanze kufikiria tutaweka nini kwenye katiba mpya kuhusu maswala ya afya. Mojawapo ni hili la kuhakikisha mwanadamu aliye tumboni kwa mama na aliye nje ya tumbo la mama yaani ameishazaliwa wanatambuliwa kuwa wote ni binadamu wanaohitaji kulindwa afya zao na kupewa huduma za afya za kuwakinga na kuwatibu. Kwenye katiba mpya tuseme bayana kuwa mtoto aliye tumboni mwa mama yake ana haki ya kulindwa na kutunzwa kama mtoto ambaye ameishazaliwa; awe na haki ya kuishi na kuwa hai kama mama yake alivyo na haki ya kuwa hai na kuishi.

Bunge la Tanzania

Tanzania ina sheria ambayo inakataza kutoa mimba. Madhumuni ya sheria hii ni kumlinda mtoto tumboni kwa mama na vile vile inalinda afya ya mama. Sasa mbona sheria haifuatwi kwa kumaanisha hatujasikia msichana au mama mmoja aliyetoa mimba akapewa adhabu?  Mbona hatujasikia hata daktari mmoja au mtu yeyote aliyesaidia katika kutoa mimba amepewa adhabu?  Sheria inasema anayesaidia kutoa mimba afungwe miaka kumi na mama au msichana anayetoa mimba afungwe miaka mitano lakini hatujasikia msichana, mama, daktari au watoa mimba wengine wamefungwa. Basi hii sheria haina maana?

Mwanadamu wa wiki 5
Lakini pamoja na mapungufu haya  siyo kwamba sheria hii haina maana. Sivyo! Kule kutofuatwa, kule kuwa hatuoni yeyote akihukumiwa vifungo vilivyotajwa na sheria vya miaka 14, 7 na 3 siyo kwamba sheria haina maana. Sheria ipo; inatukumbusha kuwa nchi yetu inaamini kuwa kila mtu hata kiumbe kilicho tumboni kwa mama kina haki ya kuishi kama ilivyo kwenye katiba ya nchi. Inaonyesha tunaamini kuweko kwa njia ya kuwasaidia walio wanyofu wasionewe na kuuawa. Kama haifuatwi basi ni kutafuta njia ya kuhimiza ifuatwe na sio kusema kuwa haina maana, haina faida.
Inawezekana ikatokea baadaye kikundi au vikundi vikataka sheria hii ibadilishwe na eti turuhusu utoaji   mimba.  Ningetaka katika makala haya kuongelea misingi fulani ya kuruhusu au kutoruhusu kutoa mimba.
Jambo la kwanza la maana ni kujua historia ya sheria za kutoa mimba ulimwenguni na hapa kwetu Tanzania. Sheria za kutoa mimba na utekelezaji wake zimekuwa zikibadilika badilika tangu enzi za kale. Sheria nyingi za mwanzo zimechukua kigezo cha kutoruhusu au kuruhusu kutoa mimba kuwa ni lini mtoto tumboni kwa mama anakuwa ni mtu hivyo kwamba ukimdhuru na kumtoa unakuwa umemdhuru na kumuua mtu.
Sheria nyingi za zamani ziliweka kigezo kuwa  uhai wa mtoto unaanza anapoanza kujitupa tupa akiwa tumboni kwa mama yaani mama anapomsikia anacheza.  Huu ni wakati mama anaweza kuisikia miondoko na mapigo ya mtoto akiwa tumboni mwake.
Badaye kwenye karne ya 18   na ya 19 watu wakafikiri zaidi na kuona kuwa mtoto aliye tumboni kwa mama ni mtu hata kabla hajaanza kupiga piga na kusukuma sukuma. Hapo basi wakatunga sheria za kutoruhusu utoaji mimba kabisa wakati wowote. Walijua na kuamini kuwa uhai wa mtoto unaanza mara mimba inapotungwa yaani mbegu na yai vinapokutana.
Ilipokuja karne ya 20 yaani karne iliyopita swali la utoaji mimba likawa siyo la sayansi tena. Likaingiliwa na wapigania haki za wanaoonewa kwa njia moja au nyingine na hata na watetezi wa haki za kina mama. Nchi nyingi za magharibi zikaanza kuruhusu utoaji mimba bila hata kufikiria anayetolewa kwenye mwili wa mama ni mwanadamu; mradi tu haki ya mama kwamba mwili ni wake na anaweza kufanya analotaka na mwili wake. Haikuzingatiwa kuwa kiumbe kilichopo tumboni mwa mama nacho  kina haki.
Hata hivyo wakati wa vugu vugu kubwa la kumkomboa mwanamke kutoka kwenye uonevu; viongozi wanaharakati huko Amerika hawakukubali utoaji mimba na walidiriki kusema, “Hata kwa sababu ipi, hata kama ni kupunguza matatizo au kwa nia ya kumuokoa mtoto kutokana na matatizo ambayo unafikiri atayapata baada ya kuzaliwa, mwanamke anayefanya kitendo cha kutoa mimba hujisikia hapo hapo na baadaye dhamira yake ikimsuta vibaya sana kwa kujua na kujisikia kuwa kitendo alichofanya ni kibaya sana.  Kitendo hiki kitamwelemea kwenye dhamira yake maisha yake yote. Yule mtu aliyemfanya akaamua hivyo na aliyemsaidia kuitoa hiyo mimba naye hupata mateso ya mara 3 ya huyu mama”

Huko Ulaya karne ya 18 utoaji mimba uliruhusiwa kabla ya mtoto tumboni kuanza kujitupa tupa yaani kabla ya mama kumsikia anacheza cheza. Baadaye kwenye karne ya 19 utoaji mimba ukakatazwa kabisa.
Tena baadaye, karne ya 20 mataifa ya magharibi yakaruhusu utoaji mimba. Katika karne mbili za 18 na 19 kuruhusu au kutoruhusu utoaji mimba kulitegemea na kuelewa kwa wanadamu kuwa kiumbe kilichopo tumboni, ubinadamu wake unaanza lini.
Karne ya 18 ilikuwa imeeleweka kuwa mimba ikiishatungwa mimba hiyo inakuwa mwanadamu wakati wa mtoto anapoanza kujitikisatikisa tumboni. Kwa hiyo walifikiri utoaji mimba kabla mtoto tumboni hajaanza kujitupa tupa; kabla mama hajamsikia akicheza cheza ilikuwa  ni sawa.  Karne ya 19, sayansi ikawa imeendelea zaidi na kuonyesha kuwa mimba ikiishatungwa hapo hapo anayetokea ni mwanadamu anayeanza safari yake ya kukua. Hapo ndipo ikabidi sheria ibadilike iseme hakuna ruksa kutoa mimba tena kwa sababu ukitoa mimba unaua binadamu. Sheria zilitungwa karne ya 19 zikikataza kutoa mimba kwani mimba ikishatungwa, anayetokea ni binadamu na unapomuua kwa utoaji mimba unaua binadamu.
Wiki ijayo tutaangalia kuwa ilipofika karne ya 20 watu wa magharibi wakarudi nyuma tena, wakakataa kuendelea kukubali jambo la kisayansi kuwa mwanadamu anaanza kuwa mwanadamu wakati mbegu na yai  wanapokutana. Wakafuta sheria za karne ya 19 zilizokataza utoaji mimba na wakatunga sheria kuruhusu utoaji mimba.
Tuandikie kama una maoni na maswali juu ya utoaji mimba; ni sawa au siyo sawa. Tuandikie uzoefu wako kama umeishatoa mimba au kama unamjua ndugu, rafiki nakadhalika aliyetoa mimba na tuambie yaliyomkuta. Barua zote ni siri bila anwani au namba ya simu. Mwandikie, Mhariri, bahimokahumba@yahoo.com P.O.box 72321 Dar es Salaamu na 0712002188 au andika hapa chini.

Washkaji;
Mshkaji 1 :Naambiwa kubadilisha sheria ya kutoa mimba huko Ulaya kulihusu vile vile haya mambo wanayozungumzia Wazungu.
Mshkaji 2 : Mambo gani?
Mshkaji 1: Naona haya kuyasema kwani kwetu siyo tu hairuhusiwi kuyafanya bali hata kuyasema. Ni haya mambo ya wenzetu huko magharibi ya wanaume eti kulala na wanaume. Huko nyuma walikuwa na sheria kuwa ukihisiwa tu na siyo wala wakukamate kuwa wewe mwanamme unalala na wanaume wanakunyonga au wanakuwekea kuni na manyasi na kukuchoma moto hapo hapo walipokukamatia. Baadaye wakabadilisha wakasema ni sawa tu wanaume walale na wanaume.
Mshikaji 2: Mamaaaa! Ni hivyo hivyo kwa sheria ya kutoa mimba kuwa huko mwanzoni ukitoa mimba wanakunyonga au kukufunga maisha na sasa ukitoa mimba haina noma!
Mshkaji 1: Kweli kumbe hizi siyo tu nchi zilizoendelea bali ni nchi zilizogeuka.


No comments:

Post a Comment