Wednesday, July 25, 2012

YAMENIKUTA

Stori za Walioambukizwa na VVU!

1. Stori ya Yohane:
Nimekuwa na matatizo ya homa za mara kwa mara, kikohozi kikavu na ukurutu kwenye ngozi. Nilihisi labda nimeishaambukizwa VVU. Mwanzo wa mwaka huu nilijisikia kudhoofika sana.  January 25 nilienda kupima nikaambiwa nina maambukizi ya VVU. Walinipima CD4 wakakuta zimeishapungua sana na ziko 100 tu.

Nilijisikia vibaya sana. Niliomba Mungu nifie mle kliniki nilikoenda kupima lakini sikufa. Nilitoka mle nimechanganyikiwa. Nilikuwa nalia nikisema, “Nitamwambiaje mke wangu kuwa nina UKIMWI. Nitamwambiaje kuwa nimeishaambukizwa na kumwambukiza VVU?  Nilipokuwa njiani naenda nyumbani niliomba nigongwe na gari lakini magari yalikuwa yananikwepa, hayapendi kunigonga. Hakuna aliyetaka kunigonga. Nilifika nyumbani, nikampigia magoti mke wangu na  kumlilia nikimwambia, “Nisamehe mke wangu nina UKIMWI.”  Sikuthubutu kusema, “Nimekuambukiza.”  Nilimwambia tu, “Nisamehe nina UKIMWI.”

Mke wangu alisikitika na kusema, “Mume wangu, umetuua, tutakufa. Mimi nimekuwa mwaminifu kwako miaka yote hii; kumbe wewe ulikuwa unatembea nje huko.” Niliomba ardhi ipasuke inimeze lakini naona Mungu alikuwa ameishaamua kuwa ni lazima niteseke kwa muda mrefu.
Kesho yake mke wangu alienda kupima na kwa muujiza ambao mpaka sasa sijaelewa, alikutwa hajaambukizwa.
Sasa imeishapita miezi mitatu natumia dawa za kurefusha maisha. Najisikia afadhali. Kinachonipa nguvu ni sapoti ninayopata kutoka kwa mke wangu, wazazi na ndugu zangu. Wamelichukulia hiji jambo kwa kunionea huruma. Wazazi na ndugu zangu hufika mara nyingi nyumbani na kukaa na sisi na kutufariji. Nina bahati kuwa nimepata janga hili miaka hii ya karne hii. Kama ingekuwa karne iliyopita, wagonjwa kama mimi walikuwa wanatengwa na kukimbiwa na familia zao na kuwaacha wafe haraka. Sasa napewa dawa, napewa sapoti na mke wangu, wazazi na ndugu zangu. Mke wangu bado ananichukulia kama mume wake na ndugu zangu kama ndugu yao.

Nilipougua kilichonisikitisha sana ni kufikiri kuwa nitakufa kabla ya mama yaani mama atanizika. Nilianza kufikiria jinsi mama atakavyosikitika kunizika. Ninajua sasa kuwa kama nikijitahidi kujizatiti kimwili na  kimawazo nitapata afya ya kuweza kuishi na kumzika mama kuliko yeye anizike mimi. Kujitahidi kutumia dawa na kula chakula na kufanya yote ninayoambiwa na waganga na familia yangu yote  nananifanya niendelee kuishi; ili tu mama asije akanizika na baada ya hapo afe kwa uchungu wa kumzika mwanae mpenzi.

Kwa vijana ambao hawajapata maambukizi ya VVU jikingeni, jikingeni  hata kama siyo kwa faida yenu lakini kwa faida ya wazazi wenu. Inauma sana mzazi anapomzika mwanae kwa uchungu. Kawaida siyo wazazi kuzika watoto ila kwa watoto kuzika wazazi.
Tuandikie taarifa fupi jinsi unavyoteseka na UKIMWI. Tutachapisha bila jina au simu namba yako kama hutataka vitokee gazetini bahimokahumba@yahoo.com 0712002188 P.O.  Box 72321 Dar es Salaam

2. Stori ya Skolastika
Mimi naitwa Scolastica. Mwaka jana nilikuwa naumwa umwa kila mara. Nakohoa, nina homa, natoka jasho na ngozi yangu ina vipele pele. Mwezi Septemba 2011 niliamua kwenda kupima nikaambiwa nimeishaambukizwa na  VVU.  Nililia sana. Niliwafikiria wanangu. Nilijua kuwa nilikuwa nafa. Nitakufa na nitawaacha wanangu wakiteseka humu ulimwenguni. Baada ya ushauri nasaha nilijisikia afadhali, nilizoea na kuendelea kupigana na ugonjwa wangu. CD4 zilikuwa zimepungua sana kwa hiyo nikaambiwa nianze dawa za kurefusha maisha mara moja. Tangu nianze kutumia dawa za kurefusha maisha najisikia vizuri. Afya yangu ni nzuri; siumwi umwi tena, nakula vizuri, nafanya mazoezi na nimenenepa kidogo.

Kuambukizwa na VVU siyo kwamba Mungu hakupendi. Wewe siyo mtu mwovu kuliko wengine. Ni kwamba tu umeambukizwa na kwa sasa ni lazima upigane na ugonjwa wako na siyo kusikitika maana kusikitika hakutawaondoa hao VVU mwilini mwako. Huu ni ugonjwa. Ulimwenguni humu kuna magonjwa mengi. Huu ni mojawapo ya magonjwa mabaya na ukiwa nao ujue tu wewe hupo peke yako. Kuna wenzako mamilioni ambao wanateseka kama  wewe. Ukipata VVU siyo kwamba umejamiana ovyo ovyo tu. Kuna ambao wanapata hata bila kujamiana, kuna ambao wanaupata bila hata kutembea nje ya ndoa. Unaweza kupata maambukizi kwa njia nyingi.

Nilimwambia mwajiri wangu kuwa nilikuwa na VVU. Bosi wangu ni mwanamke kama mimi. Alinionea huruma akanipa msaada na nikaendelea kufanya kazi.

Kuwaarifu watu kuwa unaumwa ni jambo zuri lakini chagua wale ambao unaona watakupokea, watakuonea huruma na hawatakutenga. Kama baada ya watu kujua una VVU; wakianza kukutenga, kukunyanyapaa, achana nao. Waache waishi maisha yako na wewe uishi maisha yako.
Mkakati wako ni, “Mpende akupendaye; asiyekupenda; achana naye”

Sasa najiangalia na kuishi maisha yangu siku kwa siku nikimwomba Mungu. Kila ninapoanza siku mpya; kila ninapoamka asubuhi naanza kwa kusali na  kumshukuru Mungu kuwa nimeona siku mpya kwa kuwa najua usiku uliopita wengi wanaougua ugonjwa wangu hawakuona siku hii. Ikifika jioni ninapoingia kitandani kulala namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunilinda siku nzima na kunifikisha usiku wa leo. Najua wengi walio na ugonjwa huu hawakuiona jioni ya leo. Kuna wengi wanaoumwa ugonjwa wangu  na wamekufa asubuhi hii, mchana au jioni hii. Naweka roho yangu mikononi mwa Mungu na kumwomba kama ataamua aniamshe asubuhi, lakini kama sikuamka anipokee kwake baada ya mateso haya hapa ulimwenguni.

Wiki ijayo tutasoma stori ya Aisha ambaye mpenzi wake anayesoma chuo kikuu, inavyoonekana amemwambukiza VVU
Msomaji tuandikie stori yako kama na wewe umeishawahi kuambukizwa au unamjua mtu aliyeambukizwa awe ndugu, rafiki, mfanyakazi mwenzako au jirani. Wataalamu tuandikieni mnavyomwona huyu mama na mnavyoona ugonjwa huu wa hatari: mwandikie Mhariri P. O. Box 72321 Dar es Salaam na bahimokahumba@yahoo.com  simu 0712002188 

No comments:

Post a Comment