Wednesday, July 25, 2012

Kujamiana

 

Namna ya Kusema Hapana!

ABC ni jumuisho la njia za kujikinga na maambukizi ya UKIMWI. A=Acha kujamiana yaani subiri  B= Boresha uaminifu yaani kuwa mwaminifu  na C= condoms yaani tumia kondomu. Kusubiri na kuacha siyo tu njia ya kujikinga na UKIMWI bali vile vile ni njia ya kukaa bila kujamiana ukisubiri, ukingoja wakati wako wa kujamiana ufike.

Kwa mtu msaarabu, kila kitendo kina madhumuni yake. Madhumuni ya kujamiana ni kuzaa watoto. Ili kulea mtoto na kumsomesha na kumtayarishia maisha mema ni vema watoto wakatunzwa na wazazi wawili.  Kwa hiyo mtu anaanza kujamiana na kuzaa watoto wakati ameishaoa au ameishaolewa. Kwa kuwa madhumuni ya kujamiana ni kuzaa; na kwa kuwa ni vema mtu azae wakati akiwa ameishaolewa au ameishaoa basi kujamiana kunafanyika ndani ya ndoa. Inabidi mtu asubiri mpaka anapoolewa au anapooa. Kwa wale wanaosubiri kuoa au kuolewa basi ni vema vile vile wasubiri, wasianze kujamiana.

Hata wadudu wanajamiana ili wazae

Tuangalie mfano wa wanafunzi. Watoto wa kike na wa kiume wanavunja ungo au wanabalehe wakati bado wapo shuleni. Wakishabalehe au wakishavunja ungo miili yao ina uwezo wa kuzaa. Ijapokuwa wana uwezo wa kuzaa hawawezi wakazaa kujamiana kwa sababu bado wako masomoni wakijitayarishia maisha yao ya baadaye. Kusoma ni faida yao, ya wazazi, ndugu na taifa. Hawawezi wakaanza kujamiana na kuzaa kwani bado wapo kwenye steji ya maisha ambayo ni steji ya kutayarisha maisha ya baadaye. Wakianza kujamiana hata kama hawazai tayari wameisharuka steji moja yaani wameishajitoa kwenye steji ambapo mtu anasoma na hajaanza kujamiana. Anasubiri, anangoja.

Kuanza kujamiana kuna matayarisho yaani kijana haanzi kujamiana bila kujitayarisha.  Kuna matayarisho ili mtu aanze akijua kuwa madhumuni ya kujamiana ni kwa ajili ya kuzaa na kujamiana kunaendana na majukumu ya kumdhamini unayejamiana naye, kulea mimba na kumlea na kumsomesha mtoto atakayezaliwa kutokana na kujamiana. Kijana anayeanza kujamiana bila matayarisho; bila kutayarishwa, anapata madhara mengi. Akianza kujamiana wakati akiwa bado anasoma yaani anasoma na huko ameisharuka steji hii ya masomo na kuichanganya na steji ya kujamiana, kuna uwezekano mkubwa wa kuchanganyikiwa kisaikolojia, na hata kupata mimba na Maambukizi Yanayosambazwa Kwa Kujamiana (MYKK) ambayo ni  pamoja na VVU. Wavulana nao wanaweza wakachanganyikiwa kisaikolojia, wanaweza wakawapa wasichana mimba na kuwaharibia na wao kujiharibia kabisa maisha yao. Ni vema wasichana na wavulana wasubiri kwa kujua kuwa kujamiana ni kwa madhumuni ya kuzaa. Wakisubiri  mpaka watakapofikia steji hiyo watakapoweza kusema kwa kujiamini, “Sasa nimeishatoka steji ya kusoma. Nataka kuzaa, niko tayari kuzaa, kulea na  kumsomesha mtoto kwa hiyo niko tayari kujamiana.”

Katika hali hizi za kusubiri msichana anakwepaje vishawishi? Mvulana anakwepaje vishawishi? Njia moja madhubuti ni ile ya kujua ni kwa nini asubiri. Ni kwa nini asifanye ngono. Ni kwa nini asijamiane wakati anasoma. Ni kwa nini asijamiane kabla ya kuolewa. Ajue kuna madhara gani ya kufanya ngono wakati huu akiwa shuleni au akiwa bado hajaolewa. Msichana au mvulana anafanya maamuzi. Anajiamulia kuwa anataka kuwa msichana mzuri; mvulana mzuri mpaka atakapopata mme au mke aoane naye na ajamiane naye. Mme au mke huyo atakayempata anataka kuanzia mwanzo wa mahusiano yao amuone kuwa yeye ni kijana mstaarabu, mwenye msimamo hasa kwenye maswali ya kujamiana. Atasema, “Mimi siwaruhusu watu wakanichezea mwili wangu. Mwili wangu nimeuacha na kuutunza kwa ajili ya atakayenioa au nitakayemuoa.

 Njia ya pili ya kukwepa vishawishi vya kujamiana kabla ya kuolewa au wakati mtoto anasoma ni kusema, “Bado wakati wake.” Yaani msichana au mvulana anasema kuwa kwa sasa yuko masomoni. Sasa ni wakati wa kusoma; ngono na kujamiana kutakuja baadaye. Hii ni steji ya kusoma, kujamiana kutakuja steji inayofuata nikishamaliza masomo na kuolewa au kuoa.

Kama kuna mvulana au msichana au mzee anayekushawishi unaweza ukamwambia kwa kistaarabu kuwa kwa sasa uko katika steji ya kusoma na kujitayarishia wewe mwenyewe, wazazi wako na wananchi maisha bora na bado hujaingia katika steji ya kujamiana. Mwambie angoje mpaka utakapotoka kwenye steji ya kusoma na kuingia kwenye steji ya kuolewa na kama wakati huo yuko tayari kukuoa na mkaoana na wewe uko tayari kuolewa naye na mkaoana basi wakati huo mtajamiana.

Msichana au mvulana mwenye msimamo anajua kuwa katika maisha kuna steji ya kuzaliwa, utoto, ujana, kusoma na kuolewa au kuoa. Kujamiana kunafanyika katika steji ya kuoa na kuolewa. Anaelewa kuwa ukizichanganya steji hizi yaani ukianza kujamiana wakati yupo katika steji ya kusoma unazichanganya steji hizi na kuna madhara makubwa ya kisaikolojia. Kujamiana huko kutamfanya kushindwa kufikia malengo yake ya maisha. Msichana au mvulana anayejua steji za maisha ukimshawishi ajamiane kabla ya kumaliza kusoma na hata kuolewa atakuambia, “Hapana sasa niko katika steji ya kusoma na nikimaliza masomo nitaingia katika steji ya kuolewa kujamiana na kuzaa. Nikichanganya hizi steji mbili yaani za kusoma na kujamiana nitapata madhara ya kisaikolojia ambayo ni pamoja na kushindwa kusoma, kufeli mitihani na kupata ‘division four.’ Najua kuna madhara mengi sana ya  kujamiana kabla sijamaliza masomo. Haya ni pamoja na kupata mimba na kupata Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana  ambayo ni pamoja na VVU.” Madhara ya kisaikolojia na ya kutoweza kuweka mkazo katika masomo ni makubwa zaidi kuliko hata mimba kwa kuwa yanamtesa pole pole anayejamiana na huko anasoma. Humpunguzia ufanisi wa masomo na mwisho kumkatiza au kumfelisha masomo au kumpatia ‘division four’.

Hii ni steji ya kusoma siyo ya kujamiana

Wiki ijayo tutaendelea kuzungumzia mbinu za kusema ‘hapana sitaki kujamiana’ yaani  ‘say no! to sex’

Wasomaji na hasa wazazi, vijana na wanafunzi, madaktari na wataalamu wengine tuandikie juu ya faida na mbinu za kusubiri. Tuandikie juu ya ‘experience’ yako binafsi juu ya kusubiri. Tuandike juu ya mbinu ulizotumia; juu ya ugumu au urahisi wake. Tuandikikie kama umeishapata madhara ya kutosubiri. Mpelekee barua zenu kwa Mhariri, P.O.Box 72321 Dar es Salaam, e mail bahimokahumba@yahoo.com au tupelekee meseji ya simu 0712002188. Kumbuka anwani yako na nambari ya simu vitahifadhiwa kisiri na gazeti hili. au andika hapa chini.

Washikaji

Mshikaji 1: Naona mdogo wangu huyu wa fomu 2 ameishaanza kuwa na marafiki wa kiume

Mshikaji 2: Subiri mimba za utotoni, maambukizi ya VVU, kuchanganyikiwa, kufeli mitihani au ‘division four’

Mshikaji 1: Mama anauza mihogo ya kuchoma na chapati ili kumlipia karo. Sijui nimwambie aache kumsomesha?



No comments:

Post a Comment