Hunijui kuwa niko mwilini mwako. nakutafuna pole pole. Na mwisho nitakuangusha !
Ugonjwa wa Kisukari - Dr. Tengio Urrio
Ugonjwa wa kisukari ni ugonjwa wa mwili kushindwa kuthibiti na kurekebisha kiasi cha sukari mwilini.
Leo tutaanza makala ya kwanza kati ya makala zaidi ya 30 ya kuelezea juu ya ugonjwa wa kisukari. Tutaanza kwa kuelezea kisukari ni ugonjwa gani na kwa kuwa unahusu homoni ya insulini inayotengenezwa na glandi ya pankrasi tutaanzia kwa kuelezea maana ya systima za mwili, homoni ya insulini na glandi ya pankrasi. Baadaye tutazungumzia kisukari ni nini, dalili zake, matatizo yake na matibabu yake. Tutazungumzia vile vile matatizo ya mama mjamzito wakati ana kisukari.
Tuanze makala ya kwanza kwa kusema kuwa wanafunzi wanaojifunza kuwa madaktari huanza kwa kujifunza masomo manne makubwa: anatomia (Anatomy), fisiologia (physiology), bayokemia ( biochemistry) na pathologia (pathology). La kwanza, anatomia ni somo la kufahamu muundo wa kila sehemu ya mwili wa mtu, la pili (bayokemia) na la tatu (fisiologia) ni kujua jinsi mwili unavyofanya kazi. Hujifunza, kwa mfano, namna mwili unavyomeng’enya na kuchanganya vyakula na hewa ili kuzalisha nishati ya kuendesha mwili. Katika somo la patholojia wanajifunza mabadiliko yanayotokea kwenye sehemu za mwili wakati zinapoingiliwa na magonjwa. Masomo haya manne ndiyo misingi ya kujifunza na kuelewa juu ya ugonjwa wowote pamoja na ugonjwa wa kisukari. Kwa mfano, ukitaka kuelezea juu ya ugonjwa wa kisukari huna budi kuongelea juu ya anatomia na patholojia ya kiungo kinachotengeneza homoni inayohusika kwenye ugonjwa wa kisukari. Ukitaka kuelezea kisukari kinavyodhuru jicho huna budi kuongea juu ya anatomia ya jicho.
Ili kuuelewa ugonjwa wa kisukari, hatuna budi kuyapitia masomo haya manne kwa angalau kiasi kidogo kila inapobidi.
Makundi ya magonjwa
Magonjwa yanaweza yakagawanyika kwenye makundi mawili muhimu: yanayoambukizwa na yasiyoambukizwa. Magonjwa yanayoambukizwa ni kama malaria, VVU, kisonono, safura, TB, kichocho, kichomi, kifua kikuu nakadhalika. Kundi la pili, yaani magonjwa yasiyoambukizwa lina magonjwa kama ugonjwa wa presha, kisukari, saratani na magonjwa ya moyo. Ugonjwa wa kisukari ndio ugonjwa wenye wagonjwa wengi zaidi katika kundi hili la magonjwa yasiyoambukizwa. Kuna watu karibu milioni mia moja wenye kisukari ulimwenguni. Kwa hiyo kama wewe una ugonjwa wa kisukari fahamu tu kwamba haupo peke yako kwani kuna wenzako milioni mia moja wenye ugonjwa kama wa kwako.
Systima za mwili
Mwili umejengwa na vitofali vidogo vidogo vinavyoitwa seli. Mkusanyiko wa seli za aina mbali mbali zinazoshirikiana katika kufanya shughuli moja au shughuli mbali mbali unaitwa tishu na tishu mbali mbali zikikusanyika na kushirikiana kufanya kazi moja au zaidi; mkusanyiko huu unaitwa kiungo. Mwili una viungo vingi kama ini, figo, ubongo, pankrasi nakadhalika.
Kiungo kinachohusika kwenye ugonjwa wa kisukari kinaitwa pankrasi. Kwenye kiungo hiki kuna seli na tishu mbali mbali. Selli zinazohusika na ugonjwa wa kisukari ni zile zinazotengeneza homoni ya insulini.
Kiungo kinachohusika kwenye ugonjwa wa kisukari kinaitwa pankrasi. Kwenye kiungo hiki kuna seli na tishu mbali mbali. Selli zinazohusika na ugonjwa wa kisukari ni zile zinazotengeneza homoni ya insulini.
Viungo mwilini vinaungana na kuwa na systima ambayo ni mkusanyiko wa viungo vikiungana na kufanya shughuli moja au zaidi. Mwilini kuna systima 13 ambazo ni: systima ya ubongo na neva; moyo, damu na mishipa ya damu; kupumua; kumeng’enya chakula; kinga; musuli; mifupa; kutoa taka; homoni; ngozi, uzazi na sensi
Glandi ni nini?
Kuna viungo mbali mbali mwilini moja ikiwa ni kundi ambalo linaitwa ‘glands.’ Hii ni mojawapo ya sehemu ya mwili wetu ambayo bado sijaweza kupata neno lake la Kiswahili. Kwa sasa tutafsiri neno la kitaalamu ‘glands’ kama glandi kwa Kiswahili. La maana ni kujua kuwa tunazungumzia nini tukisema mwilini kuna glandi. Mfano wa glandi ni kama zile zinazotoa machozi na zinazotoa mate. Tezi vile vile ni aina ya glandi. Kazi za glandi ni kutengeneza vimeng’enyo na homoni. Ziwa ni glandi maana hutengeneza maziwa na kuyaingiza kwenye mrija na kumpelekea mtoto anyonye kwenye chuchu ya ziwa.
Kuna aina mbili za glandi. Moja ni zile ambazo zikishatengeneza vimeng’enyo huviweka au huvifikisha kwenye mrija ambao utavipeleka huko vinakohitajika. Ya pili ni pale glandi haina mrija. Kimmeng’enyo au homoni inayotengenezwa humo huingia moja kwa moja kwenye damu. Glandi muhimu inayohusika kwenye ugonjwa wa kisukari ni pankrasi. Glandi hii inatengeneza homoni inayoitwa insulini.
Homoni ni nini?
Systima ya homoni ni mojawapo ya systima za mwili. Systima hii ni mkusanyiko wa glandi; kila moja ikitengeneza homoni muhimu za kuendesha, kurekebisha au kuthibiti shughuli maalumu kwenye mwili. Homoni ni kemikali zinazotengenezwa na viungo vya systima ya homoni. Homoni zikishatengenezwa huingia moja kwa moja kwenye damu na kupelekwa kwenye viungo lengwa zinapohitajika kuendesha, kuthibiti au kurekebisha shughuli kwenye viungo lengwa.
Mwilini kuna zaidi ya homoni 50. Kwa hiyo magonjwa yanayotokana na systima ya homoni ni mengi. Moja ya magonjwa kwenye systima ya homoni ni ugonjwa wa kisukari. Homoni inayohusika kwenye ugonjwa wa kisukari ni homoni inayoitwa insulini ambayo inatengenezwa na kiungo kinachoitwa pankrasi.
Turudie kwa kutia msisitizo kuwa moja ya systima kumi na tatu za mwili ni systima ya homoni. Humo kwenye systima ya homoni kuna glandi ambazo ni viungo vinavyotengeneza homoni. Homoni ni kemikali zinazotengenezwa na glandi na kuingia moja kwa moja kwenye damu na kupelekwa kwenye viungo lengwa zinapohitajika kuendesha, kuthibiti au kurekebisha shughuli kwenye viungo hivyo. Homoni inayohusika na ugonjwa wa kisukari inaitwa insulini na inatengenezwa na glandi inayoitwa pankrasi.
Wiki ijayo tutaelezea juu ya kiungo hiki cha pankrasi na kuelezea kinafanya kazi gani,
Wasomaji tunaomba maswali na maoni yenu kuhusu ugonjwa wa kisukari. Wataalamu tunaomba mawazo na maoni yenu mwandikieni Mhariri P.O. Box 72321 Dar es Salaam, Au changia maoni yako hapa chini.
Nashukuru sana nipata mwanga mzuri wa ugonjwa huu. naomba mwendelee kutuelimisha. je ni dawa au chakula gani au mboga au matunda gani tunatakuwa kula ili kufanya pankras ifanye kazi yake inavyotakiwa?
ReplyDelete