Wednesday, July 25, 2012

WASANII NA MICHEZO

Kifo cha Ujanani. Amy Winehouse- Nyumba ya Mvinyo
(miaka 27) Kanumba (Miaka 28)
Huko Ulaya mwaka jana tarehe  22 na 23 Juy 2011  kulitokea matukio mawili ya kihistoria na ya kusikitisha. Huko Norway tarehe 22 July 2011 kijana mmoja wa miaka 32 aliua watu  7 na kujeruhi wengine 95 kwa kuweka bomu kubwa kwenye jumba la ghorofa lenye ofisi za serekali. Baada ya kuweka bomu hilo kwenye nyumba hiyo  na wakati akingoja lilipuke alienda kwenye kisiwa kimoja ambapo  vijana walikuwa wamekusanyika kwenye mkutano akaanza kuwamiminyia risasi. Wengi wa hawa vijana walikimbilia baharini na wakati wakijitahidi kuogelea aliendelea kuwamiminia risasi wakiwa humo baharini. Ilikuwa ni gharika, ni kiama,  ni jambo la kusikitisha jinsi mtu huyu kijana wa miaka 32 alivyoamua kuua vijana wenzake na watu wengi waliokuwa kwenye hilo jumba la serekali.
Kesho yake huko Uingereza ambapo wiki hiyo habari kubwa iliyotokea ni kuwa mtu mmoja maarufu mwenye magazeti mazito ya ‘News of the World’ wandishi wake walikuwa na majambo ya kihuni ya kuingilia simu za watu na kusikiliza mazungumzo yao. Walikuwa na nguvu hizo kiasi kuwa waliweza hata kuitega simu ya Waziri Mkuu wa Uingereza na kusikiliza mambo yake ya kisiri.
Siku hiyo ya terehe 23 mwezi wa July 2011 kilitokea kifo cha msichana wa miaka 27 aliyezaliwa siyo zamani sana ila juzi juzi tu mwaka wa 1983 na siku hiyo mwaka huo wa 2011 alikuwa maiti. Ilihisiwa kuwa kifo chake kilitokana na matumizi ya pombe na madawa ya kulevya. Haikujulikana usiku huo alipofariki kama kifo chake kilitokana na kujiua au kutumia dozi kubwa mno ya madawa hayo na pombe.


Amy ‘Nyota iliyongara kwa mda mfupi’

Dada huyu mwenye sauti nzuri ambaye alikuwa amepata tuzo la ‘granny award’ alikuwa ameenda kwenye kambi  ya kutibu ugonjwa huo wa matumizi ya pombe na madawa ya  kulevya yaani ‘rehab’ kwa kizungu. Ilivyoonekana alitoka huko kabla hajapona vizuri. Kama mtu akianza kutumia madawa ya kulevya akishaenda kambini huko kutibiwa, huwa anakaa kwa mda mrefu. Lakini kwa wasanii na watu ambao wako ‘bisy ‘na ambao wamezungukwa na watu na wafanyakazi ambao kula kwao ni kutokana na kazi za msanii; huyo msanii asipoonekana hadharani kwa mda mrefu eti yuko kwenye jumba la kutibu madawa ya kulevya humshindikiza atoke humo. Kula kwao ni kutokana na huyo msanii kwa hiyo humhimiza atoke haraka huko wakimwambia, “Wewe vipi; toka huko ‘rehab’ tukatafute pesa. Unadhani sisi tutakula wapi? Tukale Polisi?”
Inavyoonekana huyu msichana Amy  Winehouse alitoka mapema huko kwenye ‘rehab’ na alipotoka hakuwa amepona vizuri na akaishia baadaye siku hiyo ya terehe 23 mwezi July 2011 aidha kujiua au kwa makosa kutumia dozi kubwa ya pombe na madawa ya kulevya. Alikufa kabisa, masikini kutokana na pombe na madawa ya kulevya. Alivyosema mshabiki mmoja ‘Taa iliyowaka kwa mwanga mkubwa imezimika mapema, na mapema sana’
Jina lake la pili  Amy ni ‘Winehouse’ maana yake nyumba ya mvinyo. Mwili wake ulikuwa ni nyumba ya mvinyo lakini ikawa nyumba ya pombe na madawa ya kulevya. Nyumba ya pombe na madawa ya kulevya haiishi  kwa mda mrefu. Ilibomoka na kuishia mapema. Mungu ailaze roho yake penye upepo mwanana.


Amy akiwa na wazazi wake



Mwaka 2004 alikuwa msichana mzuri sana. Miaka 7 badaye 2011 akawa maiti
Msanii mwingine ambaye ni mshumaa uliomulika kwa  mda mfupi ni Steven Kanumba, mcheza filamu maarufu wa Tanzania ambaye alifariki usiku wa Ijumaa kuu mwaka huu na kuzikwa Jumanne ya tarehe 12  April 2012. Kanumba alizaliwa January 1984 na kufa April 2012 akiwa na umri wa  mika 28 karibu sana na umri wa Amy  aliyefariki akiwa na umri wa miaka 27. Kwa neema yake Mwinyezi Mungu, Mwingi wa Rehema wasanii hawa wapumzike kwa Amani’

Steven Kanumba ‘mshumaa uliowaka kwa mda mfupi.’





WALEMAVU RANGI YA NGOZI


Watu Wasio na Rangi ya Ngozi, Macho na Nywele!

Tarehe 4 May ni siku ya Albino duniani. Siku ya albino duniani ni siku tunayotumia kuendeleza kuhamasisha juu ya kuelewa zaidi kuwepo kwa wenzetu wasio na rangi ya ngozi, macho na nywele na jinsi ya kushirikiana nao kuyatatua matatizo yanayoambatana na hali hii.

Baada ya siku ya albino duniani, gazeti hili linaendelea kuhamasisha ushirikiano wa kila mmoja wetu kufahamu juu ya hali hii, matatizo walio nayo walio na hali hii na kushirikiana nao katika kuyatatua. Tuongee juu ya hali hii muhimu, ‘Kutokuwa na Rangi ya Mwili, Macho na Nywele’.

Katika kushirikiana na wenzetu wasiokuwa na rangi ya ngozi macho na nywele ni muhimu tuipe hali hii jina linaloeleweka. Makala ya leo ni kuelezea ni kwa nini tuache kuiita hali hii albino, ulemavu wa ngozi, ulemavu wa rangi ya ngozi na badili yake tuiite ‘ Watu Wasio na Rangi ya Ngozi, Macho na Nywele.’
Sisi hatuna rangi ya ngozi lakini wote tu binadamu wa Mungu Mmoja Chini ya Jua Moja, Mwezi Mmoja na Mamilioni ya Nyota
Tuwaite albino?
Wanadamu wasio na rangi ya asili (melanin) tunawaita albino ambalo ni jina la Kiyunani linalomaanisha rangi. Jina hili halielezi ya kutosha hali hii kwani kusema tu albino yaani rangi haitoi maana yeyote. Hata hivyo kwa sababu tumeishawahi kulisikia mara nyingi na tumewaona albino, mtu akilisema tunajua anachosema. Lakini akilisikia mtu ambaye hajawahi kuwaona albino au mtoto mdogo kwa mara ya kwanza hana budi kuuliza maswali mengi kabla ya kuelewa hali yenyewe au watu wenyewe.

Tuwe ama tusiwe na rangi ya ngozi, wote ni ndugu
Tuwaite wenye ulemavu wa ngozi?
Jina lingine tunalosikia ni ‘ulemavu wa ngozi’ lakini kwa sababu kuna aina nyingi za ulemavu wa ngozi kusema tu ni ulemavu wa ngozi haitoshi na hata hivyo kama ni ulemavu siyo tu wa ngozi bali ni wa macho na nywele kwani hali hii inaonekana kwenye ngozi, nywele na macho. Lakini pia sioni ni kwa nini tunasisitiza sana kuwa ni walemavu kwani neno hili linaleta siyo tu unyanyapaa bali hata wao kujisikia, ‘Sisi niwalemavu, jamii inasema kuwa sisi ni walemavu’.

Tuwaite wenye ulemavu wa rangi ya ngozi?
Jina lingine tunalosikia ni ‘ulemavu wa rangi ya ngozi.’ Hapa kuna tatizo la kuwa jina hili linasisitiza sana kuwa hali hii ni ya ulemavu kiasi cha kuwafanya wahusika wajisikie ‘sisi ni walemavu.’ Hakuna sababu ya kusisitiza kuwa huu ni ulemavu kwani kwa mfano katika hali nyingine za kurithi hatukutaja kuwa zinaitwa ulemavu. Kwa mfano ugonjwa wa ‘siko selli’ ambapo mwili badala ya kuwa na haemoglobin (HB) ya kawaida inakuwa na HB tofauti, hatukuiita hali hiyo ulemavu wa damu. Kama ni kutumia neno ulemavu hapa hilo nenno lingrstahilizaidi kwa kuwa ukwelini kuwa hiyo HB ipo na iliyopo hiyo ina ulemavu. Lakini kwa ndugu zetu wasio narangi ya ngozi; ni kwamba hiyo rangi haipo kabisa. Sasa unawezaje kusema kitu ni kilemavu wakati hakipo. Kunatofauti ya kuwa na  maji machafu na kutokuwa na maji kabisa. Utasema sisi tunamaji lakini ni machafu. Utasema sisi hatuna maji. Kwa hiyo tatizo hapa siyo ulemavu wa rangi ya ngozi. Tatizo ni kuwa hiyo rangi haipo kabisa.
La maana hapa ni kutafuta jina ambalo halisisitizi kuwa ni ulemavu na ambalo linaielezea moja kwa moja hali yenyewe ili mtu bila hata kusoma makala marefu kama hii aelewe hali tunayozungumzia.

Watu wa Rangi Mbali Mbali “Mzungu, Mchina na Mwafrika

Wanadamu kwa kirangi wako aina tatu: wenye rangi nyingi (Waafrika) wenye rangi ya ngozi kidogo (Wazungu) na wasio na rangi. Kwa hiyo huoni kuwa jina sahihi la hali hii ni ‘Watu Wasio na Rangi ya Ngozi, Macho na Nywele’ (WWRNMN). Kwa kuwa hili ni jina refu na hali hii ya kutokuwa na rangi ya ngozi inajulikana kuwa inaambatana na kutokuwa na rangi kwenye  macho na nywele tungeweza tukaacha macho na nywele na kusema tu ‘Watu Wasio na Rangi ya Ngozi’ kwa kujua kuwa yeyote anayetusikia ataelewa au tutamwelewesha kuwa pamoja na kutokuwa na rangi ya ngozi, mhusika vile vile hana rangi kwenye macho na kwenye nywele. Ili kuelewa zaidi ni kwa nini tusiwaite ‘walemavu’ bali tuwaite ni ‘Watu Wasio na Rangi ya Ngozi, Macho na Nywele’ tueleze maana ya ‘ulemavu.’

Ulemavu ni nini?
Maneno yanayohusiana na ulemavu ni maneno mawili yaani udhaifu na upungufu. Mtu anapokuwa na ulemavu anakuwa na udhaifu au upungufu fulani.  Kiungo cha mwili au shughuli fulani ya mwili inakuwa imeharibika au imedhoofika. Mtu anakuwa hawezi kabisa au uwezo umepungua wa kufanya kitu fulani au shughuli fulani ambayo sasa ina kikomo, ina mipaka, ina udhaifu na mapungufu. Mtu anapata matatizo ya kushiriki katika shughuli fulani. Kushiriki kwake kunakuwa na kizuizi na mipaka.

Udhaifu au mapungufu haya yapo ya aina mbili yaani ya kurithi yaani mtu anazaliwa nayo na yanayotokea baada ya kuzaliwa. Tunaweza tukaweka ulemavu katika makundi matano: ulemavu wa viungo; wa sensi za mwili (kuona, kusikia, kugusa, kuonja kwa ulimi); ulemavu  wa ufahamu; wa akili na wa kutokana na magonjwa yaliyo kroniki. Mtu anaweza akawa na ulemavu unaoweza kuingia katika makundi zaidi ya moja na hata yote matano. Anaweza kwa mfano kuwa na ulemavu wa viungo na hapo hapo akawa na ulemavu wa sensi za mwili, ufahamu, wa  akili na utokanao na ugonjwa ambao ni kroniki.
Tuwe na rangi, tusiwe na rangi sote ni waheshimiwa

Sasa tuangalie WWRNMN wana ulemavu gani katika haya makundi matano ya ulemavu ambao unastahili kuwaita walemavu au wenye ulemavu. Wana ulemavu wa viungo? Nafikiri jibu ni ndio maana ngozi ni kiungo. Hiki kiungo hakina rangi kwa hiyo tukubali kuwa kina ulemavu pamoja na kuwa tulikataa hapo juu kusisitiza kuwa ngozi ina ulemavu. Pia wana ulemavu wa macho kwani hawaoni vizuri. Lakini bado nasisitiza kuwa, pamoja na ulemavu huu wa ngozi na macho, kuwaita walemavu wa ngozi tunasisitiza bila sababu ya msingi kuwa ni walemavu. Wana ulemavu wa sensi za mwili (sensory) kama kuona, kusikia nakadhalika? Ndio wana ulemavu wa macho na wachache wana ulemavu wa masikio lakini tunasema hata hivyo hilo halisababishi sisi kusisitiza kuwa ni walemavu. Ni ulemavu unaohitaji kupimwa na kurekebishwa kwa kutumia vifaa kama miwani ya jua, kuvaa kofia kubwa na kutumia miwani. Hatusemi kuwa haya siyo vilema lakini pamoja na kwamba ni matatizo yanayoambatana na hali hii hayatoshelezi kama sababu ya kuita hali hii ulemavu. Wana ulemavu wa ufahamu? Hapana. Wana ulemavu wa akili au wa kutokana na magonjwa ya gafla kama polio au ya kroniki? Hapana..


Sisi sote  ni ndugu

Kwa sababu tatizo la hali hii siyo ulemavu bali ni kutokuwepo kwa rangi ya ngozi, nywele na macho nafikiri msomaji utaona hakuna haja kuwaita ‘Wenye Ulemavu wa Ngozi’ Ukweli wao ni ‘Watu Wasio na Rangi ya Ngozi, Macho na Nywele.’ Na ni vema wao wasijisikie kuwa wana ulemavu na jamii isiwaone kama watu wenye ulemavu. Ndio jamii iwaone kama watu wenye mahitaji ya kipekee lakini wasisitize kuwa ni walemavu. Tunahitaji kuelimisha zaidi juu ya hali hii hasa kutokana mauaji ya hawa ndugu Wasio na Rangi ya Ngozi, Nywele na Macho.

Tangu mwaka wa 2007 watu wanaoishi na ulemavu wa ngozi  74 wameumizwa vibaya na kati yao 62 waliuawa na 12 wakabaki na madonda mabaya

Wasomaji, wataalamu na Wasio na Rangi ya Ngozi, Macho na Nywele tupeni  maswali na maoni yenu. Mwandikie Mhariri P.O Box 72321 Dar es Salaam au e mail  bahimokahumba@yahoo.com au meseji 0712 002188 au andika kwa hapa chini.

Ukatili wa Kijinsia-UWAKI

Watu wanaowapiga wake zao

Nini maana ya Ukatili Kijinsia (UWAKI)?
Ukatili wa kijinsia au UWAKI  ni ukiukwaji wa haki za binadamu ambapo mtu  kwa kutumia maungo, hisia za kujamiana au kujamiana,  au hisia za akili na kisaikolojia anamsababishia madhara mtu mwingine kwa kuwa yeye yeye mtuhumiwa anayesababisha madhara, anajisikia  au anaamini  kuwa ana uwezo na mamlaka juu ya mwathirika yaani huyo anayemthuru.
UWAKI hujumuisha vitendo anavyofanyiwa mwanamke au mwanamme  (mwathirika) bila ridhaa yake kutokana na mwanamme au mwanamke anayevifanya (mhalifu) kufikiria kuwa ana madaraka dhidi ya mwathirika.
Ukatili wa Kijinsia ni pamoja na kujamiana bila ridhaa ya mwathirika kihisia na kwa kutumia viungo vya siri, ukatili wa kimwili na wa kisaikojia, kufanya vitendo vya jadi vyenye madhara kama kukekeketa wasichana na wanawake na ukatili wa kiuchumi na wa kijamii.
Ukatili huu unawalenga watu kwa misingi ya kijinsia kwamba wao ni wanawake au ni wanaume basi wanafanyiwa vitendo hivyo.



Ukatili wa  Kijinsia ni ukatili unaotokea kati ya wanaume na wanawake ambapo kawaida anayefanyiwa ukatili ni mwanamke. Ukatili huu unatokana na kutokuwa na uwiano wa mamlaka walio nao watu wa jinsia ya kike na ya kiume, wanaume wakionekana au wakifikiri kuwa wana mamlaka zaidi dhidi ya wanawake na hata wanawake nao wakifikiri kuwa wanaume wana mamlaka zaidi kuliko wao.  Wanawake ndio hasa wanaofanyiwa ukatili kwa kuwa tu ni wanawake kwa hiyo pamoja na kuwa ukatili wa kijinsia unahusisha jinsia zote mbili, akina mama ndio hasa wanaoadhirika zaidi.  Ukatili wa kijinsia ni pamoja na kutumia maungo, ukatili  unaohusu kujamiana na unaohusu kuathirika kiakili.
Akina mama wengi na akina baba wachache wanateseka sana kimya kimya katika ndoa au mahusiano kutokana na kufanyiwa vitendo vya UWAKI. Aina za ukatili wa kijinsia ni kufanya ukatili kutumia maungo, ukatili unaohusu kujamiana, unaohusu mateso ya kiakili, unaotokea kwenye familia, ukatili kwa watoto, ubakaji,  ubakaji unaotokea kwenye mahusiano ya ndoa, unyanyasaji wa kijinsia pahala pa kazi, mashuleni na kwenye vyuo; kuingizwa kwenye shughuli za umalaya kwa nguvu,  kusafirishwa kwenda kufanyishwa kazi au umalaya na kukeketwa  kwa wasichana na akina mama.
UWAKI-Mpenzi wake alimpiga ngumi kwenye jicho ‘ pah!’
Ijapokuwa tunasema kuwa akina mama na wasichana ndio hasa wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia ukweli ni kuwa hata wanaume na vijana wa kiume wanafanyiwa ukatili wa kijinsia.
Taarifa juu ya unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa majumbani, ubakaji ndani ya ndoa na ndoa za wasichana wadogo, bado ni tatizo kubwa  hapa Tanzania.  Ukeketaji wa wasichana unaendelea kama kazi yaani ni mazoea, ikiwa ni pamoja na hata kwenye baadhi ya maeneo ya mijini.
Kuna ripoti na mashtaka machache sana ya waathirika wa Ukatili wa Kijinsia  (UWAKI)  wakiwashtaki waliowafanyia ukatili. Kati ya kesi hizi ni chache sana zinafika mahakamani na hata zile zinazofika mahakamani ni chache sana zinafikia kutolewa hukumu

Wasomaji tuandikieni mawazo yenu na uzoefu wenu juu ya unyanyasaji wa kijinsia. Wewe mwenyewe au jirani au ndugu yako amenyanyaswa au kufanyiwa ukatili wa kijinsia? Mwandikie mhariri, P.O.Box 72321 Dar es Salaam au e mail  bahimokahumba@yahoo.com au sms 0712002188
Washikaji:
Mshikaji 1: Jana jirani yangu alitusumbua  sana kwa makelele usiku. Mwanamme alikuwa analia kwa nguvu “Ntakuua! Ntakunyonga! ntakumaliza!” na huko tunasikia mangumi Pa! Pa! Pa! Pa!
Mshikaji 2:  Ndio ilivyo; sisi akina baba wakati mwingine ni wakatili. Tunawadunda sana wake zetu. Siku  moja nao watatudunda.
Mshikaji 1: Kwani aliyekuwa anadundwa ni mke basi. Tulipokimbilia nyumbani kwao tulimkuta mke amemwangusha mme wake na amemkalia tumboni; anamdunda sawa sawa. Kumbe mwanamme kwa kulia  kule alikuwa anaomba msaada lakini hakutaka majirani tujue kuwa aliyekuwa anadundwa ni yeye mwanamme.

Ameneh Bahrami sasa ni kipofu
Huko Iran mwaka wa 2004 baba  mmoja alimwagia tindi kali dada mmoja kwa kuwa eti alikataa awe mchumba wake; alimkatalia penzi kwa hiyo akamwagia tindikali machoni na kumsababishia majeraha usoni na upofu.
Huu ndio ukatili kweli kweli. Ni  UWAKI kwa kuwa huyu baba kafanya hivyo kwa kuwa ana hisia kuwa eti kwa kuwa ni mwanamme basi ana pawa (power) kuliko wanawake na mwanamke hawezi akamkatalia penzi. Kwa kuwa yeye ni mwanamme basi akimtongoza mwanamke basi ni lazima huyo mwanamke amkubalie.



 













Baada ya kumwagia tindikali na kumsabaishia makovu usoni na upofu, mahakama ya huko Irani iliamua kuwa kwa kuwa sheria za nchi hiyo zina misingi ya  jino kwa  jino basi huyu baba amwagiliwe naye tindi kali usoni kwenye macho naye apofuke. Waliamuru kuwa aende hospitali na huyu mama akishirikiana na daktari wamwekee tindi kali machoni. Adhabu  hiyo  ilikuwa itekelezwe mwezi wa  saba  mwaka wa 2011. Baba alipelekwa hospitalini na daktari akajiweka tayari kumdondoshea matone ya tindi kali kwenye macho. Mara akafika yule mama na kusema kuwa anamsamehe!

Mama huyu mwenye huruma alikuwa amesindikizwa hospitalini humo na ndugu zake wawili wakimshikia kulia na kushoto. Akionekana na makovu yake usoni na machoni na kwenye mdomo; alionekana kuwa ni mama mwenye maumivu makubwa rohoni lakini alikuwa na moyo wa huruma. Alimsamehe mbaya wake aliyemsababishia vilema vya maisha usoni na upofu.

Mama huyu anayeitwa Ameneh Bahrami alisema, “Ni vema mtu usamehe, sitaki kulipiza kisasi.’ Mbaya wake Majid Movahedi alipiga magoti na kushukuru akilia huko akiushikilia ukuta.

Sheria ya jino kwa jino inayojulikana kwa jina la ‘qisas’ (kisas) inasema kuwa pale mtu ameleta majanga basi familia yake au yeye mwenyewe huomba radhi; humwomba  aliyedhurika asamehe na kukubaliana fidia bila hivyo sheria ya jino kwa jino ichukue mkondo wake. Kwa hali hiyo mwaka wa 2010 jamaa mmoja ilibidi akatwe mkono wake kwa kuwa alitenda kosa ambalo aliyemtendea hakukubali asamehewe.

Huyu mama ambaye sasa ana vilema vya maisha, baada ya msamaha huo; huyu baba itabidi akae gerezani mpaka mahakama itakapoamua apewe adhabu gani nyingine ambayo ni pamoja na kumfidia huyu mama aliyekuwa kipofu na uso wake kuharibika.
Shirika la Haki za Binadamu (Amnesty International) wanaipinga sheria hii ya Iran ambayo inampa mtu adhabu ya kutegemea na kosa alilofanya. Kama amemfanya mtu kipofu basi naye apofuliwe. Kama amemkata mtu mkono naye akatwe mkono. Kama ameua naye auawe. Kama jicho likiharibiwa kwa kuwa alimwagia huyu mama tindi kali, basi na yeye amwagiliwe tindi kali machoni asikie maumivu makali kama aliyomsababishia aliyemjeruhi.  Shirika la ‘Amnesty International’ linasema eti pamoja na kwamba mtu amefanya kitendo cha ukatili siyo vizuri naye kumfanyia mbaya wake ukatili. Kitendo cha kinyama kikifanyika na kumjeruhi mtu ni kwamba kimeishafanyika. Kumfanyia unyama aliyekifanya hicho kitendo inakuwa ni unyama mkubwa zaidi. Siyo sawa kumfania vibaya mtu aliyefanya ubaya eti kwa kulipiza kisasi!

Msomaji hili linakuingia kichwani? na wewe unasemaje na hili? Mwandikie mhariri P.O.Box 72321 au  bahimokahumba@yahoo.com Dar es Salaam au sms 0721002188 au andika hapa chini.

Kuzaa

Vifo vya akina mama wakiwa na Mimba Vinapungua!

Utafiti wa mwaka 2010 wa Hali ya Afya ya Jamii  (UHAJ)  waonyesha mafanikio huduma za Uzazi

Utafiti wa Hali ya Afya ya Jamii 2010 (UHAJ) au kwa Kizungu DHS unaonyesha mafanikio makubwa hasa katika nyanja nne: mahudhurio  ya kliniki wakati wa kujifungua, kujifungulia hospitali, kujifungua ukisaidiwa na mhudumu wa afya yaani nesi au daktari na kupunguza vifo vya akina mama wenye mimba na wakati wa kujifungua
Kuhudhuria kliniki ya uzazi  na kupima mimba ni huduma muhimu ambapo wafanyakazi wa afya, manesi na madaktari wanampima mama na kumfuatilia ili kuyazuia matatizo yanayojitokeza wakati wa mimba, kuyatambua na kuyatibu mapema.  Kwa kupima na kufuatilia mimba kutoka inapotungwa mpaka mtoto anapozaliwa kunazuia na kupunguza matatizo yanayoweza kutokea kwa mama na mtoto wakati wa mimba, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.
Hapa kwetu Tanzania karibu akina mama wote wenye mimba, kiwango cha tisini na sita kwa mia (96%) hupimwa mimba yaani huhudhuria kliniki ya kina mama wenye mimba angalau mara moja wakati wakiwa na mimba. Utafiti wa Hali ya Afya  ya Jamii (UHAJ) wa   2004-05;  kiwango hiki kilikuwa tisini na nne kwa mia (94%) kwa hiyo UHAJ wa mwaka 2010  umeonyesha ongezeko kidogo  la  mbili kwa mia (2%). Ni vizuri kuona kuwa kuhudhuria kliniki wakati wa mimba ni moja ya huduma ambazo akina mama wana mwamko sana nazo wawe wa kijijini au wa mjini; wenye uwezo kiuchumi au wasio na uwezo wa kiuchumi,  wenye uwezo sana au wenye uwezo hafifu; wote huhudhuria kliniki wakati wakiwa na mimba
Mimba ya miezi saba

Usafi wakati wa kujifungua
Kujifungua kwenye hali ya usafi na pahala ambapo kuna huduma ya daktari au nesi kunapunguza sana uwezekano wa kupata matatizo wakati wa kujifungua yaani matatizo kwa mama na kwa mtoto. Inapunguza sana uwezekano wa kudhurika mama au mtoto. Mama akijifungulia nyumbani, akijifungulia mahali ambapo siyo pasafi; panapokosekana vifaa muhimu na wataalamu yaani daktari au nesi; mama na mtoto wana uwezekano wa kupata madhara ya kuumia na kupata maambukizi ya bakteria, virusi au fangasi.
Nusu ya mama wanaojifungua Tanzania yaani hamsini kwa mia (50%) huzalia kwenye kituo cha huduma za afya yaani hospitali, kituo cha afya au zahanati. Nusu yaani 50% huzalia  nyumbani. Hii tena ni ongezeko kutoka  UHAJ wa  2004-05 ulioonyesha kuwa arobaini na sita kwa mia (46%) ya akina mama wenye mimba  walikuwa wanazalia hospitali na 54% walikuwa wanazalia nyumbani.

Huyu mtoto amezaliwa sasa hivi
Kuna tofauti kati ya akina mama wanaozalia nyumbani na wale wanaozalia hospitali. Akina mama vijana yaani walio na mimba za mwanzo na wale wanaoishi mijini wanatumia huduma za kuzalia hospitali zaidi kuliko wale wanaojifungua mimba za baadaye, walio na umri mkubwa na wanaoishi vijijini. Inavyoonekana ni kuwa akina mama wakishaendelea kujifungua basi hupunguza kuzalia hospitali na badala yake hujifungulia nyumbani.
Akina mama wenye elimu kwa mfano wale ambao wamesoma mpaka sekondari na vyuo vikuu wana uwezekano wa mara mbili wa kujifungulia hospitali na kujifungua huko wakisaidiwa na daktari au nesi kuliko akina mama ambao hawana elimu.

Vifo vya kina mama wakati wa mimba na kujifungua
Vifo vya kina mama vinavyohusiana na uzazi ni vifo vinavyotokea wakati wa mimba, wakati wa kujifungua au miezi miwili baada ya kujifungua.
UHAJ wa 2010 ilionyesha kuwa vifo vya kina mama wakati wa mimba au kujifungua ni kiasi cha kumi na saba kwa mia (17%) ya vifo vyote vya kina mama wa miaka (15-49).  Riski ya kupoteza maisha wakati wa mimba na kujifungua ni 0.8 kwa kila akina mama 1,000
Vifo vya kinamama wakati wa kujifungua au kwa lugha ya kitaalamu ‘Maternal Mortality Ratio’ ni vifo 454 kwa kila wanawake laki moja (100,000) wanaojifungua watoto hai. Turahisishe hii takwimu kwa kusema kuwa katika wanawake 2,000 wanaojifungua watoto hai mwanamke mmoja hufariki. Kiwango hiki cha 454/100,000 ni pungufu ya kiwango kilichoonekana kwenye UHAJ wa 2004-05 ulioonyesha takwimu ya 578/100,000 na ya 1996 iliyoonyesha 529/100,000

Kama unavyoona takwimu hii na namba ya akina mama wanaokufa wakati wa mimba na kujifungua ilionyesha kuongezeka kutoka 529/100,000 mwaka wa 1996 na kuongezeka mpaka 578/100,000 mwaka wa 2004/05 na sasa mwaka wa 2010 imepungua kufikia 454 /100,000. Kwa hiyo imepungua hata kupitiliza na kuwa chini zaidi ya mwaka  1996 ilipokuwa  529/100,000. Kupungua  kwa takwimu hii ya  idadi ya vifo vya akina mama wenye mimba na wanaojifungua ni ishara nzuri kuwa jitihada zinazofanyika kupunguza vifo vya kina mama na watoto wachanga zinaanza kufanikiwa. Pamoja na kupungua idadi hii bado iko juu sana na haivumiliki. Kifo cha mzazi, hata kikiwa kimoja hakivumiliki. Ni muhimu kuziendeleza na kuzifikisha kwa wanaozihitaji hasa kwa wale wanaoishi vijijini.

Tuandike juu ya uzoefu wako wa vifo vya mama wakati wa kujifungua kama unamfahamu rafiki, jirani, mwanafamilia, mwanakijiji aliyefariki  wakati wa mimba au kujifungua. Ilikuwaje?  Mwandikie Mhariri, P.O.Box 72321 Dar  es Salaam e mail bahimokahumba@yahoo.com na sms 0712002188 au andika kwa hapa chini.

Washkaji:
Mshikaji 1: Unajua mke wangu; hii ni mimba ya tatu na anasema eti atajifungulia nyumbani. Alizalia hospitali mimba ya kwanza na hakukuwa na matatizo. Na ya pili vile vile wala hakukuwa na matatizo. Sasa anasema maana hakuna matatizo basi hii atazalia nyumbani
Mshikaji 2: Duu! Kumbe ule utafiti wa UHAJ unavyosema ni kweli kabisa kuwa wanawake wanavyoendelea kuzaa ndivyo wanavyopunguza kuzalia hospitali. Kuzalia nyumbani ni jambo la hatari kabisa maana huwezi kujua matatizo yatakapojitokeza. Wanatuambia eti matatizo wakati wa mimba yanazidi kadiri mimba zinavyozidi kuwa nyingi kwa mama mmoja. Kumbe mojawapo ya sababu za akina mama kufariki wakati wa kujifungua ni kuwa wanapoona wamezalia hospitali na hakuna matatizo, basi mimba zinazofuata wanazalia nyumbani.
Mshikaji 1: Sasa nimkubalie azalie nyumbani au azalie hospitali? Wenzake, jinsi mimba zinavyozidi kuwa nyingi ndivyo hawazalii hospitali.
Mshikaji 1: Mpeleke akazalie hospitali maana hata ikitokea huko kuwa baada ya kujifungua umerudi nyumbani bila mke na mtoto au na mtoto bila mama hutalaumiwa lakini kama hayo yakitokea hapa nyumbani! Sijui!

Utoaji mimba

Turuhusu Utoaji mimba?
Katika makala haya tunajaribu kuwaasa wasomaji waanze kufikiria tutaweka nini kwenye katiba mpya kuhusu maswala ya afya. Mojawapo ni hili la kuhakikisha mwanadamu aliye tumboni kwa mama na aliye nje ya tumbo la mama yaani ameishazaliwa wanatambuliwa kuwa wote ni binadamu wanaohitaji kulindwa afya zao na kupewa huduma za afya za kuwakinga na kuwatibu. Kwenye katiba mpya tuseme bayana kuwa mtoto aliye tumboni mwa mama yake ana haki ya kulindwa na kutunzwa kama mtoto ambaye ameishazaliwa; awe na haki ya kuishi na kuwa hai kama mama yake alivyo na haki ya kuwa hai na kuishi.

Bunge la Tanzania

Tanzania ina sheria ambayo inakataza kutoa mimba. Madhumuni ya sheria hii ni kumlinda mtoto tumboni kwa mama na vile vile inalinda afya ya mama. Sasa mbona sheria haifuatwi kwa kumaanisha hatujasikia msichana au mama mmoja aliyetoa mimba akapewa adhabu?  Mbona hatujasikia hata daktari mmoja au mtu yeyote aliyesaidia katika kutoa mimba amepewa adhabu?  Sheria inasema anayesaidia kutoa mimba afungwe miaka kumi na mama au msichana anayetoa mimba afungwe miaka mitano lakini hatujasikia msichana, mama, daktari au watoa mimba wengine wamefungwa. Basi hii sheria haina maana?

Mwanadamu wa wiki 5
Lakini pamoja na mapungufu haya  siyo kwamba sheria hii haina maana. Sivyo! Kule kutofuatwa, kule kuwa hatuoni yeyote akihukumiwa vifungo vilivyotajwa na sheria vya miaka 14, 7 na 3 siyo kwamba sheria haina maana. Sheria ipo; inatukumbusha kuwa nchi yetu inaamini kuwa kila mtu hata kiumbe kilicho tumboni kwa mama kina haki ya kuishi kama ilivyo kwenye katiba ya nchi. Inaonyesha tunaamini kuweko kwa njia ya kuwasaidia walio wanyofu wasionewe na kuuawa. Kama haifuatwi basi ni kutafuta njia ya kuhimiza ifuatwe na sio kusema kuwa haina maana, haina faida.
Inawezekana ikatokea baadaye kikundi au vikundi vikataka sheria hii ibadilishwe na eti turuhusu utoaji   mimba.  Ningetaka katika makala haya kuongelea misingi fulani ya kuruhusu au kutoruhusu kutoa mimba.
Jambo la kwanza la maana ni kujua historia ya sheria za kutoa mimba ulimwenguni na hapa kwetu Tanzania. Sheria za kutoa mimba na utekelezaji wake zimekuwa zikibadilika badilika tangu enzi za kale. Sheria nyingi za mwanzo zimechukua kigezo cha kutoruhusu au kuruhusu kutoa mimba kuwa ni lini mtoto tumboni kwa mama anakuwa ni mtu hivyo kwamba ukimdhuru na kumtoa unakuwa umemdhuru na kumuua mtu.
Sheria nyingi za zamani ziliweka kigezo kuwa  uhai wa mtoto unaanza anapoanza kujitupa tupa akiwa tumboni kwa mama yaani mama anapomsikia anacheza.  Huu ni wakati mama anaweza kuisikia miondoko na mapigo ya mtoto akiwa tumboni mwake.
Badaye kwenye karne ya 18   na ya 19 watu wakafikiri zaidi na kuona kuwa mtoto aliye tumboni kwa mama ni mtu hata kabla hajaanza kupiga piga na kusukuma sukuma. Hapo basi wakatunga sheria za kutoruhusu utoaji mimba kabisa wakati wowote. Walijua na kuamini kuwa uhai wa mtoto unaanza mara mimba inapotungwa yaani mbegu na yai vinapokutana.
Ilipokuja karne ya 20 yaani karne iliyopita swali la utoaji mimba likawa siyo la sayansi tena. Likaingiliwa na wapigania haki za wanaoonewa kwa njia moja au nyingine na hata na watetezi wa haki za kina mama. Nchi nyingi za magharibi zikaanza kuruhusu utoaji mimba bila hata kufikiria anayetolewa kwenye mwili wa mama ni mwanadamu; mradi tu haki ya mama kwamba mwili ni wake na anaweza kufanya analotaka na mwili wake. Haikuzingatiwa kuwa kiumbe kilichopo tumboni mwa mama nacho  kina haki.
Hata hivyo wakati wa vugu vugu kubwa la kumkomboa mwanamke kutoka kwenye uonevu; viongozi wanaharakati huko Amerika hawakukubali utoaji mimba na walidiriki kusema, “Hata kwa sababu ipi, hata kama ni kupunguza matatizo au kwa nia ya kumuokoa mtoto kutokana na matatizo ambayo unafikiri atayapata baada ya kuzaliwa, mwanamke anayefanya kitendo cha kutoa mimba hujisikia hapo hapo na baadaye dhamira yake ikimsuta vibaya sana kwa kujua na kujisikia kuwa kitendo alichofanya ni kibaya sana.  Kitendo hiki kitamwelemea kwenye dhamira yake maisha yake yote. Yule mtu aliyemfanya akaamua hivyo na aliyemsaidia kuitoa hiyo mimba naye hupata mateso ya mara 3 ya huyu mama”

Huko Ulaya karne ya 18 utoaji mimba uliruhusiwa kabla ya mtoto tumboni kuanza kujitupa tupa yaani kabla ya mama kumsikia anacheza cheza. Baadaye kwenye karne ya 19 utoaji mimba ukakatazwa kabisa.
Tena baadaye, karne ya 20 mataifa ya magharibi yakaruhusu utoaji mimba. Katika karne mbili za 18 na 19 kuruhusu au kutoruhusu utoaji mimba kulitegemea na kuelewa kwa wanadamu kuwa kiumbe kilichopo tumboni, ubinadamu wake unaanza lini.
Karne ya 18 ilikuwa imeeleweka kuwa mimba ikiishatungwa mimba hiyo inakuwa mwanadamu wakati wa mtoto anapoanza kujitikisatikisa tumboni. Kwa hiyo walifikiri utoaji mimba kabla mtoto tumboni hajaanza kujitupa tupa; kabla mama hajamsikia akicheza cheza ilikuwa  ni sawa.  Karne ya 19, sayansi ikawa imeendelea zaidi na kuonyesha kuwa mimba ikiishatungwa hapo hapo anayetokea ni mwanadamu anayeanza safari yake ya kukua. Hapo ndipo ikabidi sheria ibadilike iseme hakuna ruksa kutoa mimba tena kwa sababu ukitoa mimba unaua binadamu. Sheria zilitungwa karne ya 19 zikikataza kutoa mimba kwani mimba ikishatungwa, anayetokea ni binadamu na unapomuua kwa utoaji mimba unaua binadamu.
Wiki ijayo tutaangalia kuwa ilipofika karne ya 20 watu wa magharibi wakarudi nyuma tena, wakakataa kuendelea kukubali jambo la kisayansi kuwa mwanadamu anaanza kuwa mwanadamu wakati mbegu na yai  wanapokutana. Wakafuta sheria za karne ya 19 zilizokataza utoaji mimba na wakatunga sheria kuruhusu utoaji mimba.
Tuandikie kama una maoni na maswali juu ya utoaji mimba; ni sawa au siyo sawa. Tuandikie uzoefu wako kama umeishatoa mimba au kama unamjua ndugu, rafiki nakadhalika aliyetoa mimba na tuambie yaliyomkuta. Barua zote ni siri bila anwani au namba ya simu. Mwandikie, Mhariri, bahimokahumba@yahoo.com P.O.box 72321 Dar es Salaamu na 0712002188 au andika hapa chini.

Washkaji;
Mshkaji 1 :Naambiwa kubadilisha sheria ya kutoa mimba huko Ulaya kulihusu vile vile haya mambo wanayozungumzia Wazungu.
Mshkaji 2 : Mambo gani?
Mshkaji 1: Naona haya kuyasema kwani kwetu siyo tu hairuhusiwi kuyafanya bali hata kuyasema. Ni haya mambo ya wenzetu huko magharibi ya wanaume eti kulala na wanaume. Huko nyuma walikuwa na sheria kuwa ukihisiwa tu na siyo wala wakukamate kuwa wewe mwanamme unalala na wanaume wanakunyonga au wanakuwekea kuni na manyasi na kukuchoma moto hapo hapo walipokukamatia. Baadaye wakabadilisha wakasema ni sawa tu wanaume walale na wanaume.
Mshikaji 2: Mamaaaa! Ni hivyo hivyo kwa sheria ya kutoa mimba kuwa huko mwanzoni ukitoa mimba wanakunyonga au kukufunga maisha na sasa ukitoa mimba haina noma!
Mshkaji 1: Kweli kumbe hizi siyo tu nchi zilizoendelea bali ni nchi zilizogeuka.


Kujamiana

 

Namna ya Kusema Hapana!

ABC ni jumuisho la njia za kujikinga na maambukizi ya UKIMWI. A=Acha kujamiana yaani subiri  B= Boresha uaminifu yaani kuwa mwaminifu  na C= condoms yaani tumia kondomu. Kusubiri na kuacha siyo tu njia ya kujikinga na UKIMWI bali vile vile ni njia ya kukaa bila kujamiana ukisubiri, ukingoja wakati wako wa kujamiana ufike.

Kwa mtu msaarabu, kila kitendo kina madhumuni yake. Madhumuni ya kujamiana ni kuzaa watoto. Ili kulea mtoto na kumsomesha na kumtayarishia maisha mema ni vema watoto wakatunzwa na wazazi wawili.  Kwa hiyo mtu anaanza kujamiana na kuzaa watoto wakati ameishaoa au ameishaolewa. Kwa kuwa madhumuni ya kujamiana ni kuzaa; na kwa kuwa ni vema mtu azae wakati akiwa ameishaolewa au ameishaoa basi kujamiana kunafanyika ndani ya ndoa. Inabidi mtu asubiri mpaka anapoolewa au anapooa. Kwa wale wanaosubiri kuoa au kuolewa basi ni vema vile vile wasubiri, wasianze kujamiana.

Hata wadudu wanajamiana ili wazae

Tuangalie mfano wa wanafunzi. Watoto wa kike na wa kiume wanavunja ungo au wanabalehe wakati bado wapo shuleni. Wakishabalehe au wakishavunja ungo miili yao ina uwezo wa kuzaa. Ijapokuwa wana uwezo wa kuzaa hawawezi wakazaa kujamiana kwa sababu bado wako masomoni wakijitayarishia maisha yao ya baadaye. Kusoma ni faida yao, ya wazazi, ndugu na taifa. Hawawezi wakaanza kujamiana na kuzaa kwani bado wapo kwenye steji ya maisha ambayo ni steji ya kutayarisha maisha ya baadaye. Wakianza kujamiana hata kama hawazai tayari wameisharuka steji moja yaani wameishajitoa kwenye steji ambapo mtu anasoma na hajaanza kujamiana. Anasubiri, anangoja.

Kuanza kujamiana kuna matayarisho yaani kijana haanzi kujamiana bila kujitayarisha.  Kuna matayarisho ili mtu aanze akijua kuwa madhumuni ya kujamiana ni kwa ajili ya kuzaa na kujamiana kunaendana na majukumu ya kumdhamini unayejamiana naye, kulea mimba na kumlea na kumsomesha mtoto atakayezaliwa kutokana na kujamiana. Kijana anayeanza kujamiana bila matayarisho; bila kutayarishwa, anapata madhara mengi. Akianza kujamiana wakati akiwa bado anasoma yaani anasoma na huko ameisharuka steji hii ya masomo na kuichanganya na steji ya kujamiana, kuna uwezekano mkubwa wa kuchanganyikiwa kisaikolojia, na hata kupata mimba na Maambukizi Yanayosambazwa Kwa Kujamiana (MYKK) ambayo ni  pamoja na VVU. Wavulana nao wanaweza wakachanganyikiwa kisaikolojia, wanaweza wakawapa wasichana mimba na kuwaharibia na wao kujiharibia kabisa maisha yao. Ni vema wasichana na wavulana wasubiri kwa kujua kuwa kujamiana ni kwa madhumuni ya kuzaa. Wakisubiri  mpaka watakapofikia steji hiyo watakapoweza kusema kwa kujiamini, “Sasa nimeishatoka steji ya kusoma. Nataka kuzaa, niko tayari kuzaa, kulea na  kumsomesha mtoto kwa hiyo niko tayari kujamiana.”

Katika hali hizi za kusubiri msichana anakwepaje vishawishi? Mvulana anakwepaje vishawishi? Njia moja madhubuti ni ile ya kujua ni kwa nini asubiri. Ni kwa nini asifanye ngono. Ni kwa nini asijamiane wakati anasoma. Ni kwa nini asijamiane kabla ya kuolewa. Ajue kuna madhara gani ya kufanya ngono wakati huu akiwa shuleni au akiwa bado hajaolewa. Msichana au mvulana anafanya maamuzi. Anajiamulia kuwa anataka kuwa msichana mzuri; mvulana mzuri mpaka atakapopata mme au mke aoane naye na ajamiane naye. Mme au mke huyo atakayempata anataka kuanzia mwanzo wa mahusiano yao amuone kuwa yeye ni kijana mstaarabu, mwenye msimamo hasa kwenye maswali ya kujamiana. Atasema, “Mimi siwaruhusu watu wakanichezea mwili wangu. Mwili wangu nimeuacha na kuutunza kwa ajili ya atakayenioa au nitakayemuoa.

 Njia ya pili ya kukwepa vishawishi vya kujamiana kabla ya kuolewa au wakati mtoto anasoma ni kusema, “Bado wakati wake.” Yaani msichana au mvulana anasema kuwa kwa sasa yuko masomoni. Sasa ni wakati wa kusoma; ngono na kujamiana kutakuja baadaye. Hii ni steji ya kusoma, kujamiana kutakuja steji inayofuata nikishamaliza masomo na kuolewa au kuoa.

Kama kuna mvulana au msichana au mzee anayekushawishi unaweza ukamwambia kwa kistaarabu kuwa kwa sasa uko katika steji ya kusoma na kujitayarishia wewe mwenyewe, wazazi wako na wananchi maisha bora na bado hujaingia katika steji ya kujamiana. Mwambie angoje mpaka utakapotoka kwenye steji ya kusoma na kuingia kwenye steji ya kuolewa na kama wakati huo yuko tayari kukuoa na mkaoana na wewe uko tayari kuolewa naye na mkaoana basi wakati huo mtajamiana.

Msichana au mvulana mwenye msimamo anajua kuwa katika maisha kuna steji ya kuzaliwa, utoto, ujana, kusoma na kuolewa au kuoa. Kujamiana kunafanyika katika steji ya kuoa na kuolewa. Anaelewa kuwa ukizichanganya steji hizi yaani ukianza kujamiana wakati yupo katika steji ya kusoma unazichanganya steji hizi na kuna madhara makubwa ya kisaikolojia. Kujamiana huko kutamfanya kushindwa kufikia malengo yake ya maisha. Msichana au mvulana anayejua steji za maisha ukimshawishi ajamiane kabla ya kumaliza kusoma na hata kuolewa atakuambia, “Hapana sasa niko katika steji ya kusoma na nikimaliza masomo nitaingia katika steji ya kuolewa kujamiana na kuzaa. Nikichanganya hizi steji mbili yaani za kusoma na kujamiana nitapata madhara ya kisaikolojia ambayo ni pamoja na kushindwa kusoma, kufeli mitihani na kupata ‘division four.’ Najua kuna madhara mengi sana ya  kujamiana kabla sijamaliza masomo. Haya ni pamoja na kupata mimba na kupata Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana  ambayo ni pamoja na VVU.” Madhara ya kisaikolojia na ya kutoweza kuweka mkazo katika masomo ni makubwa zaidi kuliko hata mimba kwa kuwa yanamtesa pole pole anayejamiana na huko anasoma. Humpunguzia ufanisi wa masomo na mwisho kumkatiza au kumfelisha masomo au kumpatia ‘division four’.

Hii ni steji ya kusoma siyo ya kujamiana

Wiki ijayo tutaendelea kuzungumzia mbinu za kusema ‘hapana sitaki kujamiana’ yaani  ‘say no! to sex’

Wasomaji na hasa wazazi, vijana na wanafunzi, madaktari na wataalamu wengine tuandikie juu ya faida na mbinu za kusubiri. Tuandikie juu ya ‘experience’ yako binafsi juu ya kusubiri. Tuandike juu ya mbinu ulizotumia; juu ya ugumu au urahisi wake. Tuandikikie kama umeishapata madhara ya kutosubiri. Mpelekee barua zenu kwa Mhariri, P.O.Box 72321 Dar es Salaam, e mail bahimokahumba@yahoo.com au tupelekee meseji ya simu 0712002188. Kumbuka anwani yako na nambari ya simu vitahifadhiwa kisiri na gazeti hili. au andika hapa chini.

Washikaji

Mshikaji 1: Naona mdogo wangu huyu wa fomu 2 ameishaanza kuwa na marafiki wa kiume

Mshikaji 2: Subiri mimba za utotoni, maambukizi ya VVU, kuchanganyikiwa, kufeli mitihani au ‘division four’

Mshikaji 1: Mama anauza mihogo ya kuchoma na chapati ili kumlipia karo. Sijui nimwambie aache kumsomesha?